Marekani kupambana na uuzaji wa bidhaa bandia

Mamlaka ya forodha Marekani ikionyesha bidhaa bandia zilizokamatwa.

Rais Trump aelekeza wizara ya usalama wa ndani kushirikiana na mwanasheria mkuu na wizara ya biashara na idara nyingine kwa pamoja kuchunguza tatizo hilo

Waraka umesainiwa na rais wa Marekani Donald Trump siku ya Jumatano ili kupambana na uuzaji wa bidhaa bandia kupitia kwenye mitandao kama vile Alibaba, Amazon na eBay.

“Rais ameamua ni wakati wakusafisha soko holela la bidhaa bandia na usafirishaji haramu alisema Peter Navarro, msaidizi wa rais na mkurugenzi wa ofisi ya biashara na sera za uzalishaji.

Licha ya kwamba hatua za Trump hazipelekei kuchukuliwa hatua mara moja dhidi ya watengenezaji na wauzaji wa bidhaa hizi za bandia, ambazo ni kuanzia dawa za binadamu hadi viatu vya michezo vyenye majina ya hali ya juu, inaelekeza wizara ya Usalama wa ndani ya Marekani kushirikiana na mwanasheria mkuu , mwakilishi wa biashara wa Marekani na wizara ya biashara na idara nyingine za serikali, ili kuweza kwa pamoja kuchunguza tatizo hilo na kuwasilisha ripoti na mapendekezo ndani ya siku 210.

Hatujui ni kiasi gani cha bidhaa bandia kinaendelea kuiingizwa alisema Navarro.

Imetayarishwa na Sunday Shomari.