Vanessa Mdee na Mrembo Tunda kuhojiwa na polisi Jumatatu

Kamanda wa Polisi wa Dar es Salaam, Simon Siro

Msanii Vanessa Mdee pamoja na mrembo Tunda Kimaro wametakiwa kufika kituo cha polisi cha kati Dar es Salaam, Jumatatu kwa ajili ya kuhojiwa kuhusiana na madawa ya kulevya.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dar es Salaam Simon Siro ameeleza kuwa kamata kamata hiyo ilitokea wiki hii ambapo watu watano waliwekwa rumande, hivyo idadi ya wale tayari wako mikononi mwa polisi kufikia 17.

Wakati polisi wanaendelea na zoezi hilo tayari limekwisha wahusisha zaidi ya watu 10 ambao walitajwana Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda Alhamisi kuhusika na biashara ya dawa za kulevya na wanahojiwa na polisi.

Mkuu wa mkoa ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda amewataja baadhi ya askari polisi na raia wanaoshukiwa kujihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya mkoani, huku akiamuru wengine kufika kituo kikuu cha polisi kwa mahojiano

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Makonda alisema usiku wa kuamikia Alhamisi akiwa na baadhi ya askari na vyombo vingine vya usalama wamefanya operesheni ya madawa ya kulevya usiku kucha katika baadhi ya maeneo na kubaini kuwepo uuzwaji wa dawa hizo hadharani.

Amewataja wanaoshikiliwa na Polisi ni pamoja na Said Masoud Linna au Alteza, Ahmed Hashim Ngahemela au Peti Man, Bakari mohamed Khelef pamoja na Mohamed Nasor Mohamed.

Hata hivyo baadhi ya wasanii akiwemo Wema Sepetu, Rachel ,Khaleed Mohammed (TID), Samir Kheri (Mr Blue) ,dogo Hamidu na Yahaya Mlawa (babu wa kitaa) wakitakiwa wajisalimishe polisi.