Madaktari wamepanga kuanza mgomo kuanzia Januari 6, 2023 endapo serikali haitakuwa imetekeleza makubaliano hayo.
Makubaliano yanahusu kutatua uhaba wa madaktari kwa kuajiri madaltari kadhaa, kuwaongezea madaktari mishahara, kuwapandisha vyeo, utekelezaji wa bima ya afya na kuboresha mazingira ya kazi ikiwemo kununua vifaa vya kutosha vya matibabu.
Serikali za majimbo 47 zimelazimika kuingia katika mazungumzo ya dharura na madaktari ili kuzuia mgomo huo.
Katika mazungumzo yaliyofanyika Jumatano wiki hii (Dec 28, 2022), kati ya baraza la magavana na wawakilishi wa muungano wa madaktari, wamekubaliana kuanza hatua za haraka za mazungumzo ili kuepusha mgomo.
Mkutano pia unajadili kukamilishwa kwa makubaliano mapya ya mkataba wa makubaliano ya mwaka 2021-2025.
Baraza la magavana linaongozwa na mwenyekiti wa kamati ya afya ambaye ni gavana wa jimbo la Tharaka Nithi Muthomi Njuki na gavana wa Nairobi Johson Sakaja ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya Leba.
Yaliyojiri katika mazungumzo
Wanaoshiriki mazungumzo wameangazia zaidi kuhusu
- Uingiaji upya wa mazungumzo kuhusu mkataba wa pamoja wa 2021-2025
- Mfumo wa utekelezaji kamili wa mkataba wa 2017-2021
- Kiasi cha nyongeza ya mshahara wa kiwango cha chini
- Utatuzi wa suala la uchelewashaji wa malipo ya mishahara na marupurupu kwa madaktari
- Makato ya pesa yasiyolipwa kisheria na malipo ya bima
- Bima ya matibabu kwa madaktari wote
- Kuajiriwa kwa madaktari wasiokuwa na kazi rasmi
- Ukosefu wa vifaa inavyohitajika kazini
- Mafunzo ya baada ya kuhitimu na kupandishwa cheo kwa madaktari
- Mikopo ya magari na ya nyumba
- Ajira ya madaktari kwa masharti ya kudumu na pensheni miongoni mwa mengine.
Ugumu wa utekelezaji wa mkataba kati ya serikali na madaktari
Kupitia matakwa ya siku thelathini waliyokuwa wameipa serikali 47 za kaunti na serikali kuu ya Kenya, madaktari hao wameeleza kuwa walilazimika kufanya hivyo kutokana na ugumu wa utekelezaji wa mkataba wa pamoja unaondoa vizuizi kadhaa vinavyolemaza maboresho ya sekta ya afya nchini Kenya.
Dkt Davji Atellah, Katibu mkuu wa Muungano wa Madaktari nchini Kenya, KMPDU amesema kwamba ni sharti serikali kuu na serikali za kaunti zitoe suluhisho ili kuboresha sekta ya afya la sivyo watasusia kazi na kuanza maandamano kote nchini Kenya.
“Kama serikali kuu na serikali za kaunti hawataki tufanye mgomo, basi watekeleze yale ambayo tumekuwa tukidai ili tufanye kazi katika mazingira rahisi katika hospitali za umma kote nchini.”
Kuna hofu kubwa kwamba huenda wagonjwa katika hospitali za umma wakahangaika sana kote nchini Kenya iwapo mazungumzo kati ya madaktari na maafisa wa serikali hayatafanikiwa .
Waziri wa Afya Susan Wafula Nakhumicha, amewasihi madaktari kuendelea kushiriki mazungumzo ili kuhakikisha kwamba huduma ya afya haiathiriki.
Migomo ya madaktari imekuwa ikitokea kila mwaka nchini Kenya, sababu za mgomo zikiwa zile zile na ambazo zimekosa suluhu kutoka kwa kila serikali inayoingia madarakani. Kila mara, serikali huwa inasema kwamba haina pesa za kutosha kutimiza matakwa ya madaktari.
Imetayarishwa na Kennedy Wandera, VOA, Nairobi