Madai ya ulaghai yaghubika BBI Kenya, baadhi ya vipengele viliongezwa kisiri

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta (katikati), Naibu wa rais William Ruto (kushoto) na kiongozi wa upinzani Raila Odinga (kulia) wakati wa uzinduzi wa ripoti ya BBI, Nairobi, Kenya

Hisia mbali mbali zinendelea kutolewa Kenya, kufuatia madai kwamba ulaghai ulifanyika kwa ripoti ya maridhiano inayofahamika kama BBI, kwa kuingiza sehemu nyingine ambazo hazikuafikiwa na jopo maalum lililoandika ripoti hiyo.

Makundi mbali mbali pia yamesemwa kwamba maoni yao hayakujumulishwa kwenye ripoti hiyo iliyozinduliwa na rais Uhuru Kenyatta mwezi uliopita.

Madai ya kuongezwa kwa sehemu kwenye ripoti hiyo ambazo jopo halikukubaliana yametolewa na Meja mstaafu John Seii, ambaye ni mojawapo ya wanachama katika jopo lililoandika ripoti hiyo.

Hatua hiyo imezua maswali chungu nzima kuhusu uhalali wa ripoti hiyo ambayo imetajwa na rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga, kuwa kinga ya matatizo ya Kenya.

Seii, amesema kwamba jopo hilo halikujadili na kuafikiana kuongezwa kwa maeneo bunge 70 mapya kama njia ya kukinga usawa wa kijinsia.

“Tulishangazawa sana wakati suala la maeneo bunge lilipowasilishwa na kuthibitishwa na wote walioenda Naivasha katika kikao cha wabunge.” Amesema John Seii katika mahojiano na runing ya KTN, akiongezea kwamba “hapakuwepo maafikiano kati ya wanajopo kuweka nafasi ya waziri mkuu na manaibu wake watakaoteuliwa na rais, kwa sababu hiyo ingeongeza mzigo kwa raia wa Kenya wanaolipa ushuru.”

Hata hivyo, madai ya Seii yamepingwa na wakili Paul Mwangi ambaye pia ni katibu wa jopo hilo.

Kupitia ujumbe wa twitter, Mwangi ameandika kwamba “madai ya Seii hayana msingi wowote na anachosema ni ulaghai.” Ameendela kuandika kwamba “yaliyoandikwa kwenye ripoti ya BBI yaliafikiwa na wanachama wote na kuweka sahihi bila kusurutishwa.”

Makundi mbali mbali ya kijamii pia yamedai kwmaba maoni yao hayakutiliwa maanani kwenye ripoi hiyo.

Viongozi kutoka jamii za wafugaji wa kuhamahama wamesema kuwa sharti maoni yao yajumulishwe katika ripoti hiyo la sivyo, wataipinga.

Naibu wa rais William Ruto na viongozi wengine wanaendelea kushinikiza kujumulishwa kwa maoni ya kila mtu ndipo ripoti hiyo ipitishwe.

Utata mkubwa kwenye tipoti hiyo unahusu marekebisho kwenye tume ya uchaguzi, mahakama na maeneo bunge.

Mchakato wa kukusanya sahihi milioni moja kutoka kwa raia wa Kenya unatarajiwa kukamilika mwezi Desemba.

Tume ya uchaguzi inatarajiwa kuthathmini sahihi hizo kufikia Januari kabla ya mswada wa marekebisho ya katiba kuwasilishwa katika mabunge ya majimbo kupigiwa kura.

Imetayarishwa na mwandishi wetu wa Nairobi Kennedy Wandera.