Madai ya mafao kwa watu wasio na kazi yalipungua kiasi nchini Marekani wiki iliyopita, wizara ya kazi iliripoti Alhamis.
Taifa lenye uchumi mkubwa duniani lipo kwenye njia ya kufufua uchumi wake kutoka kwenye janga la virusi vya Corona lakini hata hivyo wafanyakazi wapya 411,000 waliopunguzwa kazi waliwasilisha maombi ya fidia ya kukosa ajira wiki iliyopita ikiwa chini ya maombi 7,000 kutoka idadi iliyotathminiwa wiki moja kabla, wizara ya kazi nchini Marekani ilisema.
Ilikuwa ni wiki ya pili mfululizo kwamba idadi ya kila wiki ilikuwa laki nne. Idadi inabaki juu ya wastani kwa kila wiki ikiwa chini ya laki tatu hapo mwaka 2019 kabla ya janga hilo kuingia Marekani mnamo Machi mwaka 2020.
Magavana wa majimbo na maafisa wa manispaa wamekuwa wakiondoa masharti ya virusi vya Corona katika kesi nyingi wakiruhusu biashara kwa mara ya kwanza katika kipindi cha mwaka mmoja, kufunguliwa tena jumla kwa ajili ya wateja. Hatua hiyo inaweza kusababisha kuajiriwa wafanyakazi wengi zaidi.
Zaidi ya asilimia 56 ya watu wazima wote nchini Marekani, hivi sasa wamepata chanjo kamili dhidi ya virusi vya Corona ili kuimarisha hali ya uchumi kuponya japokuwa kasi ya uchomaji chanjo imeshuka sana kutoka mahala ilipokuwa wiki kadhaa zilizopita.
Maafisa katika majimbo mengi hivi sasa, wanatoa motisha mbali mbali za kuwahamasisha watu wasiopata chanjo kwenda kupatiwa chanjo pamoja na fursa ya kuingia kwenye bahati nasibu yenye faida kwa pesa taslim na kulipiwa ada kwa masomo katika chuo.
White House ilisema wiki hii kwamba haitarajii Marekani itafikia lengo la Rais Joe Biden la asilimia 70 ya wamarekani watu wazima kupatiwa angalau dozi moja ya chanjo dhidi ya virusi vya Corona ifikapo siku ya uhuru hapo Julai nne. Idadi hiyo kwa sasa bado ipo kwenye asilimia 65.6.