Macron aliomba bunge kujadili kuhusu muungano

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron

Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron ameliomba bunge kujadiliana kuhusu muungano mpana wa kile alichokiita “taasisi za jamhuri” za nchi hiyo.

Anatarajia kumaliza hali ya sinto fahamu baada ya uchaguzi ambao haukutoa muafaka wa moja kwa moja.

“Ninaomba pande zote za kisiasa zinazojitambua katika taasisi za jamhuri, utawala wa sheria, demokrasia ya bunge, mwelekeo wa Ulaya na ulinzi wa uhuru wa Ufaransa, kuanza mazungumzo ya kweli na ya haki ili kujenga umoja thabiti, utakao akisi vyama vingi,” Macron amesema.

Mpangilio huo ulionekana kuundwa ili kukitenga chama cha mrengo wa kulia cha National Rally cha Marine Le Pen. Pia haijumuishi mwanasiasa wa mrengo mkali wa kushoto Jean-Luc Melenchon.

LFI inaunda kiasi kikubwa cha muungano wa mrengo wa kushoto wa New Popular Front, au NFP.

NFP ilikuwa na viti vingi zaidi katika bunge la taifa Jumatano. Kundi la kati la Macron limekuwa la pili, na RN ya tatu.