Ushahidi wa kisayansi ulioandikwa katika mfululizo wa makala zilizowasilishwa na Shirika la Afya Duniani wiki hii unaonyesha athari mbaya za mabadiliko ya hali ya hewa katika hatua muhimu za mzunguko wa maisha ya binadamu.
“Hatua hizi hutoa ushahidi muhimu wa kisayansi kuhusu afya za wanawake wajawazito, watoto wachanga, watoto, vijana na wazee zinavyoathiriwa na uchafuzi wa hewa, na hatari tofauti za hali ya hewa, ikijumuisha moto wa msituni, mafuriko, na joto kali, Anayda Portela, mwanasayansi katika idara ya afya ya mama, mtoto mchanga, na wazee katika WHO, alisema katika mkutano wa waandishi wa habari huko Geneva.
Ushahidi huu ni muhimu sana, kwa sababu unaonyesha hatari za kiafya zinazoongoza kwa kila moja ya vikundi hivi kwa matukio haya tofauti ya hali ya hewa, Portela alisema. Alieleza kuwa mkusanyiko wa makala zilizochapishwa katika Journal of Global Health unaonyesha kuwa hatari za afya zinazohusiana na hali ya hewa “zimepuuzwa sana” kwa vijana na wazee na wakati wa ujauzito, na athari hizo mbaya, mara nyingi ni za kutishia maisha”.
Utafiti huo umegundua kuwa hatari za asili zinazohusiana na hali ya hewa zina “athari kubwa katika afya ya akili na kimwili” wakati wa ujauzito, na kwa vijana na wazee.