Kupitia barua iliyotiwa saini na Maaskofu 11, wamelalamikia kile wamesema ni kuminywa kwa uhuru wa demokrasia kufuatia mashitaka yaliyofuguliwa dhidi ya viongozi 6 wa upinzani, wanahabari pamoja na wanaharakati.
Baraza hilo ndilo linaloongoza kanisa Katoliki nchini humo, chini ya uongozi wa Ignatius Chama, ambaye ni askofu mkuu wa dayosisi ya Kasama, ambaye amesema kuwa, “Tuna wasiwasi kuhusu ukamataji wa wanasiasa na polisi wa Zambia. Kinachohuzunisha zaidi ni muda mrefu ambao polisi wanazuilia watu kinyume cha sheria.”
Chama ameomba mamlaka kuondoa pendekezo la mabadilko ya sheria za uhalifu bungeni, na badala yake kuzingatia mashauriano. Kulingana na mtandao wa bunge, msuada uliowasilishwa unalenga kuongeza adhabu kwa wale wanaopatikana na hatia ya matamshi yenye chuki.
Wakati wa kuwasilishwa kwa msuada huo hapo Juni, Rais Hakainde Hichilema alisema kuwa baadhi ya watu katika jamii wanaeneza maneno yenye chuki dhidi ya baadhi ya makabila, suala alilosema linaweza kupelekea ghasia. Alisema kuwa sheria iliopendekezwa itahakikisha kuwa wanaopatikana na hatia wanapewa adhabu ya kutosha ili wengine wajifunze.
Muungano wa Upinzani wa Kwacha Alliance au UKA unaojumuisha vyama 10 vya kisiasa umeambia VOA kwamba kanisa Katoliki limejidhihirisha kuwa sauti ya wanyonge nchini Zambia. Jackson Silavwe ni msemaji wake.
Msemaji mkuu wa serikali Cornelius Mweeta ameambia wanahabari Jumanne kwamba serikali inaendelea kutathmnini barua iliowasilishwa na maaskofu hao.
Agosti mwaka huu, afisa wa ngazi ya juu wa haki za binadamu kwenye UN alitoa ripoti ikisema kuwa ukamataji wa viongozi wa upinzani nchini Zambia umepelekea athari kubwa dhidi ya uhuru wa kujieleza, kutangamana na kukusanyika nchini humo, pamoja na kudumaza juhudi za ukuaji wa taasisi za kidemokrasia.