Viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki walifikia makubaliano ya mwezi Novemba ya kutaka kundi la M23 ambalo wapiganaji wake wanatoka kabila la Watutsi, kuacha vita na kuondoka sehemu ambazo wamekuwa wakishikilia.
Kulingana na ofisi ya rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Felix Tshisekedi, waasi hao walitakiwa wameshaondoka ifikapo Januari 15.
Waasi wa M23 wameshutumiwa kwa kushindwa kuheshimu makubaliano hayo na rais wa DRC ameuambia mkutano wa uchumi duniani unaoendelea Davos, Uswizi kwamba waasi hao wamekataa kuondoka kutoka sehemu walizokuwa wanazidhibithi.
“Licha ya shinkizo kutoka kwa jumuiya ya kimataifa, kundi hilo limekataa kuondoka. Bado lipo katika sehemu hizo,” amesema Tshisekedi.
“Wanajifanya kwamba wanaondoka, lakini hawaondoki. Wanazunguka tu na kujiimarisha katika sehemu nyingine na kuishi katika miji ambayo wamekuwa wakiidhibithi,” ameongezea.
Lakini msemaji wa kundi la M23 Lawrence Kanyaka amepuuza madai hayo akisema kwamba “Rais Tshisekedi hana jingine la kusema. Serikali ndio haitaki kuheshimu mkataba na inaendelea kutoa silaha kwa makundi mengine ya waasi.”
Maandamano yanataka wanajeshi wa EAC kushambulia M23
Makundi ya kutetea haki za kiraia yameitisha maandamano ya mjini Goma na kulalamimia namna utekelezaji wa mkataba wa waasi wa M23 kuondoka. Waandamanaji wanasema hawajaona mabadiliko yoyote.
Waandamanaji wanataka jeshi la Jumuiya ya Afrika Mashariki kuondoka DRC.
“Tunataka jeshi la Jumuiya ya Afrika Mashariki kuondoka mjini humu au kuanza vita vikali dhidi ya kundi la M23. Warudi nyumbani kwao ama waanzishe vita dhidi ya adui,” amesema Gloire Bagaya, mmoja wa waandamanaji mjini Goma.
Mashambulizi ya kundi la M23 yamesababisha zaidi ya watu 450,000 kukoseshwa makao na kupelekea mgogoro wa kidiplomasia kati ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo na Rwanda.
DRC inadai kwamba Rwanda inawaunga mkono waasi wa M23, madai ambayo yametolewa pia na wataalam wa Umoja wa Mataifa. Rwanda inakanusha madai hayo.