Kwa mujibu wa shirika la habari la AP, hali hiyo imepelekea watu kukumbatia chanjo kwa wingi licha ya kuzikataa katika siku za nyuma.
Maelfu ya maambukizi mapya ya corona yametangazwa katika wiki za karibuni baadhi ya mataifa yakitangaza idadi kubwa zaidi tangu janga hilo kutokea mwaka uliopita.
Wakazi ambao mwanzoni, walikuwa na wasiwasi kuhusu chanjo, kutokana na taarifa potovu kwenye mitandao ya kijamii, sasa wanasemekana kupanga foleni ndefu ili kupata chanjo kwenye mataifa ya Liberia, Nigeria, Ghana na Senegal.
Uhaba wa chanjo umechelewesha zoezi la utoaji chanjo kwenye mataifa 54 ya Afrika wakati chanjo milioni 82 zikiwa tayari zimetolewa kufikia sasa.
Hata hivyo hiyo ni asilimia 10 pekee ya asilimia 30 ya chanjo zinazohitajika kutolewa kufikia mwisho wa 2021, amesema Dkt Matshidiso Moeti ambaye ni mkurugenzi wa WHO tawi la Afrika.