Polisi nchini Tanzania, walisema siku ya Jumapiloi kuwa wana ushahidi wa kutosha wa kumkamata na kukumfungulia mashtaka kiongozi wa upinzani Seif Shariff Hamad, ambaye ni katibu mkuu wa chama cha CUF, kwa kile walichokiita uhaini.
Inspekta mkuu wa polisi nchini Tanzania, Ernest Mangu, alinukuliwa na gazeti la ‘The Citizen’ akisema kuwa vitendo na maneno aliyoyatamka Hamad yameandikwa na kwamba huenda akakamatwa na maneno hayo kutumiwa dhidi yake.
Gazeti hilo lilisema kuwa matamshi hayo ya inspekta mkuu wa polisi yamejiri siku chache tu baada ya naibu wa katibu mkuu wa jumuiya ya madola, Josphine Ojiambo, kusema akiwa mjini London kwamba jumuiya hiyo ina mipango ya kufanya mazungumzo na serikali ya Tanzania na chama cha CUF ili kutafuta suluhisho la mzozo wa kisiasa unaokumba kisiwa cha Zanzibar.