Kansela Scholz hajasema ikiwa Ujerumani itakubali kuipa Ukraine vifaru hivyo vya vitani, lakini shirika la habari la Reuters limemnuku akisema maamuzi kama hayo yatachukuliwa kwa ushirikiano na washirika ikiwemo Marekani.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema haondoi uwezekano wa kutuma vifaru aina ya Leclerc nchini Ukraine. Hata hivyo ameonya kuwa kutuma vifaru hivyo kusije kuhatarisha usalama wa Ufaransa au kuzidisha vita kati ya Ukraine na Russia.
Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza James Cleverly Jumapili alisema katika mahojiano na kituo cha Sky News kuwa angependelea kuona Waukraine wakipata vifaa kama kifaru aina ya Leopard 2.
Mbunge Mrepublican McCaul ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya bunge ya masuala ya nje amekiambia kituo cha ABC kwamba Marekani inapaswa kutoa vifaru vizito aina ya Abrahams kwa Ukraine ili kuhamasisha Ujerumani kutuma kwa upande wake vifaru aina ya Leopard 2.