Mwendesha mashtaka mkuu nchini Kenya amesema mashtaka yataanza kusikilizwa mara moja juu ya washukiwa hao waliotajwa katika upelelezi uliofanywa na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Mkosa ya Jinai, ingawaje majina ya watu hao hayajatangazwa kwa umma mpaka hivi sasa.
Televisheni binafsi ya Citizen na nyengine ya K24 zimeripoti kuwa mkurugenzi wa taasisi hiyo ya vijana, Richard Ndubai, alikamatwa pamoja na maafisa wengine. Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai amesema katika ujumbe aliouandika kupitia simu kuwa watu 17 wanashikiliwa.
Televisheni ya Citizen imeripoti kuwa afisa wa ngazi ya juu katika wizara ya huduma ya umma, huduma ya watoto na jinsia, amejisalimisha polisi akiwa ameandamana na mawakili wake.
Vyombo vya habari nchini Kenya vimesema shilingi bilioni 10 ($99 milioni) zilikuwa zimeibiwa kupitia madai ya uongo na malipo kadhaa yaliyotolewa kwa kampuni moja iliyokuwa inatoa huduma kwenye taasisi hiyo ya vijana.
Shirika la habari la Reuters halikuweza kumpata Ndubai, ambaye yuko rumande, ili kupata maoni yake, na pia hawakuweza kupata maoni ya wakili wake.
Pamoja na ahadi ya Rais Uhuru Kenyatta kutokomeza ufisadi alipokuwa amechaguliwa mara ya kwanza 2013, wapinzani wake wanasema kuwa amekuwa akisuasua katika kuwashughulikia maafisa wa ngazi ya juu.
Wamesema kuwa pale tu majina makubwa yatakapo fikishwa mahakamani na kuhumiwa kifungo ndipo utakuwa mwisho wa utamaduni wa kuvunja sheria.