M23 wametuhumiwa kwa mauaji ya Watoto, utekaji nyara, unajisi na kutumia Watoto kama wapiganaji

Wapiganaji wa kundi la waasi la M23 wakiwa katika mji wa Goma, mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo

Ripoti ya umoja wa mataifa kuhusu vita vya waasi mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo inawatuhumu waasi wa kundi la M23 kwa mauaji ya Watoto na akina mama, kuwateka watu nyara, unajisi na mateso mengine ya raia.

Ripoti hiyo vile vile inasema kwamba kundi la M23 limewalazimisha Watoto kuwa wapiganaji wake.

Imechapishwa baada ya wataalam wake kutembelea Rutshuru, mkoa wa Kivu kaskazini, ambapo waasi wa M23 wanashikilia.

Kuna zaidi ya makundi 120 ya waasi mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, yanayopiganana na wanajeshi wa serikali.

Kundi la M23 limetajwa pia katika ripoti ya awali ya umoja wa mataifa kwamba linapokea msaada kutoka kwa serikali ya Rwanda inayoongozwa na rais Paul Kagame.

Serikali ya Rwanda imekanusha madai hayo mara kadhaa.

Marekani, Ufaransa, Ujerumani na Ubelgiji zimetaka Rwanda kuacha kusaidia kundi la waasi la M23.

Kundi hilo lilitangaza wiki iliyopita kuondoka sehemu ambazo limekuwa likishikilia za Bunagana.

Kundi hilo lilijitokeza mapema mwaka huu baada ya kuwa kimya kwa miaka kadhaa.

Ripoti ya umoja wa mtaiafa inasema kwamba kando na kuwanyanyasa raia, waasi wa M23 wanalazimisha wakaazi kulipa kodi.

Wanakusanya dola 27,000 kila mwezi kwenye mpaka wa Bunagana karibu na Uganda.

Kundi hilo limekuwa likifutilia mbali ripoti zote zinazodai kwamba linatekeleza mauaji, utekaji nyara na maovi mengine mashariki mwa jamhuri ya kidemokrasia ya Congo.

Waasi wa Allied democratic forces – ADF

Ripoti ya umoja wa mataifa vile vile inaonyesha mashaka na oparesheni ya jeshi la Uganda kupambana na kundi la waasi la Allied democratic forces ADF mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo.

Oparesheni hiyo iliyoanza mwezi Novemba 2021 inatekelezwa kwa ushirikiano wa jeshi la Uganda na jeshi la Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo - FARDC.

Ripoti ya Umoja wa mataifa inasema kwamba licha ya oparesheni hiyo, kundi la ADF limeendelea kutekeleza mashambulizi na limejiimarisha zaidi.

Jeshi la umoja wa mataifa limekuwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo kwa muda kwa ajili ya kulinda amani lakini hawajafanikiwa kurejesha utulivu mashariki mwa DRC.

Lakini msemaji wa jeshi la Uganda Brig Felix Kulayigye ameambia gazeti la Uganda la Daily monitor kwamba umoja wa mataifa haustahili kukosoa oparesheni ya UPDF dhidi ya waasi DRC.

Ripoti ya umoja wa mataifa inasema kwamba tangu mwezi April 2022, kundi la ADF limeua watu 370, na kuteka nyara watu 374 wakiwemo Watoto.

Ripoti inasema kwamba waasi hao walichukua vitu vya raia kimabavu, kuchoma moto nyumba kadhaa, na hospitali pamoja na kuiba dawa.

Waasi hao walishambulia sehemu za Bahema-Boga na Banyali-Tchabi, Ituri pamoja na kusini mashariki mwa Beni.

Licha ya oparesheni ya Shujaa, inayoongozwa na jeshi la UPDF, ripoti ya umoja wa mataifa inasema kwamba ADF imeendelea kuimarisha mashambulizi kadhaa hasa katika sehemu za Beni, Kivu kaskazini na Kusini mwa Ituri.