Lulu akutwa na hatia ya kuua bila kukusudia

Elizabeth Michael (Lulu) akitoka mahakamani.

Msanii na muigizaji wa filamu wa Tanzania Elizabeth Michael, maarufu kama Lulu aliyekuwa anakabiliwa na tuhuma za kumuua bila kukusudia mpenzi wake Steven Kanumba amekutwa na hatia.

Wazee wa Baraza ambao ni washauri wa mahakama kuu kanda ya Dar es salaam, waliafikiana kumkuta Lulu na hatia ya kuua bila kukusudia.

Lulu aliwasili mahakamani hapo asubuhi ya Alhamisi kusikiliza shauri ya kesi yake ambayo ilikabidhiwa kwa baraza la wazee.

Vyanzo vya habari nchini Tanzania vimewanukuu wazee wa baraza wakitoa misimamo ifuatayo wakati kesi hiyo inasikilizwa.

Mzee wa kwanza Alisema: Nimeridhika na ushahidi uliotolewa kwa pande zote mbili, Elizabeth ameua bila kukusudia kutokana na marehemu kuwa na mwili mkubwa”.

Mzee wa pili pia Alisema; Naweza kusema kuwa Elizabeth hakuua kimakusudi aliua bila kukusudia”.

Mzee wa tatu pia alimalizia; Lulu ameua bila kukusudia”.

Baada ya majibu hayo ya wazee wa baraza, Jaji Sam Rumanyika anategemea kutoa hukumu yake tarehe 13 Novemba mwaka huu.

Bado haijajulikana kwa sheria za Tanzania Lulu atapata hukumu gani mpaka sasa. Kutokana na kosa hilo anaweza akapata kifungo cha miaka kadhaa jela au hata faini