Lipumba avilaumu vyama vya upinzani Tanzania

Ibrahim Lipumba kiongozi wa chama cha CUF

MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Ibrahim Lipumba amefananisha kitendo cha baadhi ya vyama vya siasa kususia uchaguzi wa ubunge Jimbo la Longido mkoani Arusha na maeneo mengine nchini Tanzania ni sawa na kumsusia nguruwe shamba la mihogo.

Aliongeza kuwa kitendo cha kususia uchaguzi kilichofanywa na baadhi ya vyama vinavyounda Umoja wa Katiba mpya (Ukawa) ulifanywa kwa kurupuka na ni kuiminya demokrasia ya vyama vingi na kuwanyima haki wananchi kutumia demokrasia yao.

Profesa Lipumba alisema hayo kitongoji cha Longido, Arusha Jumamosi wakati akimnadi mgombea ubunge wa chama hicho, Kisiyongo Meseyeki Ole Kurya ili achaguliwe kuwa mbunge wa jimbo hilo.

Kwa mujibu wa Lipumba CUF iliposhiriki uchaguzi mara ya kwanza mwaka 1995 haikufanikiwa kupata kiti hata kimoja cha ubunge Tanzania Bara, lakini kamwe hawakuweza kususa uchaguzi wa mwaka 2000 na ndio maana wameshiriki uchaguzi wa ubunge Longido na udiwani Arusha Mjini.

Pia ameeleza kuwa mwaka 2015 CUF ilishinda kwa kishindo uchaguzi Zanzibar lakini ukachakachuliwa na uliporudiwa chama hicho kilisusa na matokeo yake walipoteza viti vyote vya uwakilishi na ubunge Zanzibar na kuanza kujilaumu kwa kususa bila kuangalia mambo ya msingi.

Lipumba amedai kuwa kususa kwa Ukawa katika chaguzi za Longido na kwingineko ni sawa na mkulima kulisusia shamba la mihogo kwa nguruwe.

Amefafanua kuwa kususia huko ni kupelekea bidhaa hiyo iendelee kuliwa na nguruwe na ndio maana Chama Cha Mapinduzi(CCM) kinafurahia hilo kama vile nguruwe alivyoachiwa shamba.

“Demokrasia ya kweli haitafutwi kwa kususasusa ila hutafutwa kwa mikiki ya kushiriki chaguzi zote zinazotangazwa na Tume ya Uchaguzi(NEC) na kutoa salamu kwa wananchi kuwa haki haiko sawa kwa wote kwa kuwaeleza katika mikutano ya hadhara ya kampeni,” amesema mwenyekiti huyo.

Mwenyekiti ameongeza kuwa demokrasia ndani ya vyama kuifikia kikamilifu inahitaji mchakato wa muda mrefu na mchakato huo unahitaji uvumilivu na ujasiri mkubwa na sio kususa.

“Watanzania watashindwa kuvielewa vyama vya siasa vya upinzani kama vitaendelea kususa chaguzi mbalimbali hapa nchini,” amesema.

Amekiri kuwa demokrasia nchini Tanzania ina mapungufu tangu kuanzishwa mfumo wa vyama vingi, hivyo aliwataka viongozi wa vyama vya upinzani kuacha kususia uchaguzi kwani siyo suluhisho la kudai Demokrasia kwani ni hatua hasi inayopelekea CCM kuendelea kutawala nchini.