Bei ya mafuta na dhahabu ilipanda ghafla Jumatatu kutokana na wasiwasi mkubwa uliowakumba wawekezaji kutokana na vurugu za kisiasa nchini Libya, ambayo ni muuzaji mkubwa wa mafuta.
Bei ya mafuta ghafi ya Brent katika soko la London, linalotoa taswira ya biashara hiyo duniani, ilipanda kwa zaidi ya asilimia mbili na kufikia dola 105 kwa pipa. Hiyo ni bei kubwa zaidi tangu mwaka 2008. Bei ya mafuta ghafi nchini Marekani pia ilipanda ghafla, lakini bado sio kama London.
Bei ya dhahabu imepanda kwa zaidi ya dola 13 na kuzidi dola 1,400 kwa ratili moja, ikiwa ni mara ya kwanza katika wiki saba, kutokana na wawekezaji kutafuta mahala salama pa kuwekeza fedha zao.
Libya ni nchi ya 12 kwa ukubwa kwa usambazaji mafuta duniani. Kwa mujibu wa idara ya nishati ya kimataifa, nchi hiyo inazalisha kiasi cha mapipa milioni 1.6 ya mafutaghafi kwa siku, kiasi cha asilimia mbili ya dai la mafuta duniani.