Watekaji nyara wa ndege ya Libya wajisalimisha

Watu wakishuka kutoka kwenye ndege iliyotekwa ya shirika la ndege la Afriqiyah kwenye uwanja wa ndege wa Malta.

Waziri mkuu wa Malta, Joseph Muscat amesema kupitia akaunti yake ya Twitter Ijumaa kwamba watekaji nyara wa ndege ya Libya wamejisalimisha kwa vyombo vya dola.

Katika mfululizo wa Tweets, amesema watekaji hao walishuka kutoka kwenye ndege na wahudumu walibakia ndani yake.

Ndege hiyo ilielekezwa Malta, kilomita 500 kaskazini mwa pwani ya Libya baada moja wa watekaji nyara kuwaambia wahudumu kuwa wanalo bomu la mkononi. Ndege hiyo ilikuwa kwenye safari zake za kawaida nchini Libya.

Awali, abiria hao walishuka chini na mabasi yaliletwa ndani ya uwanja kuwaondoa hapo. Picha za televisheni hazikuonyesha ishara zozote za mapambano au ving’ora.

Taarifa za awali zimesema mmoja wa watekaji nyara aliwaambia wahudumu kuwa yeye ni “mfuasi wa Gaddafi”

Haikuwa bayana ni kitu gani watekaji hao walikuwa wanataka. Kiongozi huyo wa zamani wa Libya Muammar Gaddafi aliuwawa katika machafuko ya mwaka 2011, na nchi hiyo ikaingia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Afisa wa juu wa Usalama wa Libya ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba Ijumaa asubuhi wakati ndege iko safarini rubani aliwafahamisha kitengo cha mawasiliano ya anga katika uwanja wa ndege wa Mitiga kuwa ndege imetekwa nyara.

“Rubani aliripoti kwa waendesha mawasiliano mjini Tripoli kwamba walikuwa wametekwa, na baada ya hapo wakapoteza mawasiliano,” afisa huyo alisema akiombwa asitajwe jina.

“Rubani huyo alifanya bidii kujaribu kuwashawishi watue katika uwanja wa ndege kwa salama lakini walikataa.”

Ndege hiyo ilikuwa inasafiri kutoka Sebha kusini magharibi mwa Libya ikielekea Tripoli safari ambayo kwa kawaida inachukua zaidi ya saa mbili. Ndege hiyo Afriqiyah Airways ni mali ya serikali ya Libya.

Kisiwa kidogo cha Malta kilichoko katika bahari ya Mediterranean, ambacho ni mwanachama wa Jumuiya ya Ulaya, kipo kilomita takriban 500 kaskazini mwa Tripoli.

Tukio kubwa la utekaji nchini Malta lilitokea mwaka 1985, pale wa-Palestina walipoiteka ndege ya Egyptair. Makamando wa Misri waliivamia ndege na baadhi ya watu waliuwawa.