Kura zahesabiwa Tanzania, Upinzani unadai kuwepo udanyanyifu

Madai ya kuwepo kura bandia yametolewa na wagombea wa upinzani hasa katika vituo vya kupigia kura jijini Dar-es-salaam, Kigoma na Pangani Tanga, japo mwenyekiti wa tume ya uchaguzi amesema madai hayo hayajathibitishwa.

Kura zinaendelea kuhesabiwa nchini Tanzania baada ya uchaguzi ambao kwa kiasi kikubwa, maafisa wa uchaguzi wanasema umekuwa mtulivu.

Kata nne hazijafanya uchaguzi wa madiwani kutokana na sababu mbalimbali.

Mwenyekiti wa tume ya taifa ya uchaguzi NEC, Jaji Mstaafu, Semistocles Kaijage amesema kwamba kata nne zilizoshindwa kufanya uchaguzi wa ngazi ya madiwani ni kutokana na kwamba wagombea katika kata tatu walifariki dunia.

Uchaguzi umeahirishwa katika kata ya nne baada ya kukosekana karatasi za kupigia kura.

Madai ya kuwepo kura bandia yametolewa na wagombea wa upinzani hasa katika vituo vya kupigia kura jijini Dar-es-salaam, Kigoma na Pangani Tanga, japo mwenyekiti wa tume ya uchaguzi amesema madai hayo hayajathibitishwa.

Mgombea ubunge kwa tiketi ya chama cha chadema katika jimbo la Kawe, Halima Mdee alikamatwa napolisi na kuachiliwa baadaye alipodai kwamba kulikuwa na udanyanganyifu ulikuwa unaendelea katika baadhi ya vituo vya kupigia kura.

Picha za video ambazo zimeekwa kwa mitandao ya kijamii na watu mbalimbali wakiwa sehemu mbalimbali za Tanzania, zinaonyesha wafuasi wa upinzani kizichoma moto karatasi za kura zinazodaiwa kuwa bandia.

Mawasiliano kupitia kwa mitandao ya kijamii imeathiriwa kwa kiasi kikubwa kutokana n aukosefu wa internet na kulazimu baadhi ya watu kutumia VPN.

Huduma ya internet, whatsapp, twitter na mitandao mingine imesitishwa kabisa katika baadhi ya sehemu za nchi.

Watumiaji wa internet wamesema tukio la internet kupungua kasi yake wakati wa uchaguzi ni la kwanza kuwahi kushuhudiwa nchini humo.

Mgombea wa urais Tanzania bara Tundu Lissu amesema kwamba dosari nyingi zimejitokeza katika vituo vingi vya kupigia kura, Pamoja na kuwepo vijisanduku vya kupigia kura ambavyo tayari vilikuwa vimeshajazwa kura kabla ya zoezi la kupiga kura kuanza.

Ameandika kwenye ukurasa wake wa twiter kwamba mawakala wa chama chake wamezuiwa kuingia katika vituo vya kupigia kura.

Lisu ni mshindani mkuu wa rais wa sasa John Magufuli anayegombea mhula wa pili madarakani.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara Mack Njera amesema kwamba zoezi la upigaji kura limefanyika vizuri na kwa amani na kusisitiza kwamba usalama umeimarishwa ili kufanikisha zoezi hilo.

Kiongozi wa chama cha upinzani cha ACT Wazalendo Zitto Kabwe, ameandika kwenye ukurasa wake wa twiter kwamba wamekamata kura kadhaa ambazo tayari zilikuwa zimepigwa kabla ya vituo kufunguliwa.

“Tumekamata kura ambazo zimeshapigwa katika Jimbo langu la Uchaguzi. Tutazuia kila mbinu yao chafu. Kila mbinu yao chafu,” ameandika Kabwe.

Tume ya uchaguzi imesema tuhuma zote sio za kweli na sinastahili kupuuzwa.

Matokeo ya kura za madiwani na wabunge yanatarajiwa kuanza kutolewa wakati wowote.

Matokeo ya kura za urais anatarajiwa kuchukua mda kutolewa.

Kwa mujibu wa katiba ya Tanzania, matokeo ya kura za urais hayapingwi mahakamani.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC