Kundi la ISIS ladai kuhusika na shambulizi la Baghdad

Kundi la kigaidi la ISIS, limedai kuhusika katika mashambulizi mawili ya mabomu ya kujitoa mhanga, katikati mwa Baghdad jana alhamisi.

Shambulizi hilo lililotokea ndani ya soko lenye idadi kubwa ya watu, liliua watu 32 na kujeruhi wengine 110.

Limetajwa kuwa shambulizi baya zaidi kuwahi kutokea katika muda wa miaka mitatu.

Kulingana na wizara ya mambo ya ndani, mshambuliaji wa kwanza alijifanya kuwa mgonjwa na kuvutia wasamaria wema kumsaidia, na baada ya watu wengi kukusanyika mahali hapo, alilipua bomu alilokuwa amevaa.

Shambulizi la pili lilitokea pale watu walipokimbilia mahali hapo kuwasaidia waliokuwa wamejeruhiwa.

Shambulizi hilo ni la hivi karibuni kutokea Baghdad tangu Januari mwaka 2018.