Kundi la G7 leo Jumapili lilisema muda unazidi kuyoyoma kwa Iran kukubali makubaliano ya kuzuia malengo yake ya nyuklia na kuionya Russia kuhusu madhara ya kuivamia Ukraine.
Mawaziri wa mambo ya nje kutoka mataifa tajiri sana duniani walifanya mkutano wa siku mbili mjini Liverpool, kaskazini-magharibi mwa Uingereza, wakitaka kuwasilisha msimamo thabiti wa pamoja dhidi ya vitisho ulimwenguni.
Kuhusu Iran, mwenyeji wa G7 Uingereza ilisema mazungumzo yaliyoanza tena mjini Vienna yalikuwa nafasi ya mwisho ya Jamhuri ya Kiislam ya kufika kwenye meza ya mashauriano na azimio zito. Bado kuna wakati kwa Iran kuja na kuukubali mkataba huu Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, Liz Truss aliuambia mkutano wa waandishi wa habari wakati mazungumzo yalipokamilika.
Mazungumzo yalianza tena Alhamis iliyopita kujaribu kufufua makubaliano yam waka 2015 kati ya Iran na mataifa yenye nguvu duniani, ambapo Marekani ilijiondoa wakati wa utawala Rais wa wakati huo Donald Trump mwaka 2018.