Katika mabadiliko ya kihistoria, Waislam na wa Marekani wenye asili ya Kiarabu walivunja utiifu wa miongo miwili kwa chama cha Democratic, na kuzigawanya kura zao zilizo nyingi, kati ya Rais mteule Donald Trump na wagombea wa chama cha tatu katika uchaguzi wa rais wa Jumanne.
Kuondoka kwa kundi hilo kulichangiwa na hasira juu ya jinsi utawala wa Biden ulivyoshughulikia vita huko Gaza, ambapo kulimsaidia Trump kushinda majimbo muhimu wakati alipomshinda makamu rais Kamala Harris katika kinyang'anyiro cha kuwania urais katika White House.
Chini ya nusu ya wapiga kura wa Kiislamu waliopiga kura walimuunga mkono Harris, kulingana na kura ya maoni ya wapiga kura zaidi ya 1,000 iliyotolewa na Council on American Islamic Relations (CAIR)- Baraza la Mahusiano ya Kiislamu Marekani.
Wengi wao walipiga kura kwa mgombea wa chama cha tatu au Trump, alisema Robert McCaw, mkurugenzi wa masuala ya ndani ya serikali wa CAIR.