Kaimu Spika ya Bunge la Brazil amebatilisha uamuzi wa kufutilia mbali utaratibu wa kumfungulia mashtaka Rais Dilma Rousseff na wala hakuna maelezo yaliotolewa kutokana na kubadilishwa kwa uamuzi wake.
Kutokana na Spika Waldir Maranhao kubatilisha uamuzi huo aliofanya jana Jumatatu, sasa mashitaka didhi ya Rais yanaweza kuendelea. Iwapo baraza la Senate litaendelea na hatua hiyo, utawala wake Rousseff huenda ukafika kikomo ambapo aliyekuwa mshirika wake wa karibu wa kisiasa na aliyegeuka kuwa hasimu, Makamu Rais Michel Temer atachukua mamlaka.
Rousseff anatuhumiwa kutumia uwezo wake kuficha hali ya kiuchumi nchini humo ili kuweza kushinda katika uchaguzi wa rais wa mwaka 2014. Rais huyo amelaumu wapinzani wake akiwemo Temer ambaye anachunguzwa kutokana na tuhuma za ufisadi kwa kupanga njama dhidi yake.