Kuachiliwa huru wafungwa wa kisiasa Rwanda na shinikizo la jumuiya ya kimataifa

Upinzani nchini Rwanda

Wachambuzi wa siasa za Rwanda wanasema kwamba hatua ya Baraza la Mawaziri kuwaachia huru wafungwa Jumamosi inafuatia tetesi kuwa jumuiya za kimataifa imeitaka Rwanda kuwaachilia huru wapinzani wa Rais Paul Kagame.

Vyanzo vya habari vinaripoti kuwa hii inatokana na serikali ya Rwanda kuwa imedhamiria kuwa mwenyeji wa mkutano wa viongozi wa nchi za madola mwaka 2020.

Pamoja na kuachiliwa wafungwa 2140 Jumamosi wanasiasa wa upinzani wanaendelea kushinikiza kuachiliwa kwa mwanasiasa Diana Rwigara kuachiliwa huru.

Kati ya hao waliopewa msamaha Jumamosi ni Kizito Mihigo na Victoire Ingabire Umuhoza, na wengine kati ya hao hukumu zao zilibadilishwa kwa uwezo aliopewa Rais kufuatia maombi yao ya hivi karibuni juu ya kupewa msamaha Juni 2018.

Diana, ambaye alikuwa mpinzani mkuu wa Paul Kagame mwaka 2017, anazuiliwa gerezani kwa mashtaka ya kuhepa kulipa kodi na makosa mengine ya uchaguzi.

Diana ni binti wa aliyekuwa mfadhili mkuu wa chama kinachotawala nchini Rwanda RPF, aliyeuawa katika ajali ya barabarani, mwaka 2015.

Ibara ya 245 na 246 ya sheria dhidi ya uhalifu nchini Rwanda (sheria namba 30/2013 ya tarehe 24/5/2013) inaruhusu kuachiliwa huru kwa wafungwa ambao wametumikia robo tatu ya kifungo chao, wanaotumikia kifungo cha miaka isiyozidi 5, au robo mbili ya hukumu inayozidi miaka 5 (au miaka 20 kwa wanaotumikia hukumu ya maisha gerezani).

Masharti ya kuachiliwa huru kwa msamaha ni pamoja na mfungwa kuonyesha kwa dhati kwamba amebadilika kitabia na anaahidi kwa uaminifu kwamba atabadilika kabisa. Mfungwa pia anaweza kuachiliwa huru endapo anaugua ugonjwa usiokuwa na tiba na amefanyiwa vipimo vya kutosha na kamati ya kiafya inayojumulisha madaktari 3 wanaotambuliwa kote nchini.

Ibara ya 109 ya Katiba ya Rwanda inaeleza kwamba "rais wa jamhuri ya Rwanda ana mamlaka ya kusamehe kulingana na utaratibu uliowekwa na sheria na baada ya kufanya mashauriano na mahakama ya kilele".

Kulingana na taarifa ya serikali, ifuatayo ndio idadi ya wafungwa walisamehewa kulingana na wilaya wanakotoka;

Bugesera 23
Nyarugenge 447
Musanze 149
Gicumbi 65
Nyanza 63
Rubavu 158
Rwamagana 455
Nyagatare 24
Huye 484
Muhanga 207
Ngoma 35
Rusizi 7
Nyamagabe 23

Imetayarishwa na Mwandishi wetu Kennes Bwire, VOA, Washington DC.