Korea Kaskazini yalaumu Marekani na Korea Kusini kwa uchokozi.

Picha tofauti za mashambulizi ya silaha ya hivi karibuni kutoka Korea Kaskazini.

Korea kaskazini imesema Jumatatu kwamba majaribio yake ya silaha katika siku za karibuni yamechochewa na mazoezi hatari ya kijeshi ambayo yamekuwa yakifanywa na  Marekani pamoja na korea kusini.

Hayo yamejiri wakati kusini ikisema kwamba imepata baadhi ya mabaki ya silaha zilizorushwa na kaskazini karibu na ufukwe wake. Wiki iliyopita Kaskazini ilirusha makombora kadhaa yakiwemo yale ya masafa marefu, wakati Marekani na korea kusini walipokuwa wakifanya mazoezi ya kijeshi ya siku 6, yaliyomalizika Jumapili.

Jeshi la Korea kaskazini limesema kwamba mazoezi hayo kwa jina Vigilant Storm ,yalikuwa ya kichokozi yakilenga kuongeza hali ya taharuki katika eneo la peninsula ya korea. Korea kusini na Marekani wamesema kwamba kuna uwezekano wa Pyongyang, wa kufanya jaribio la silaha za nyuklia likiwa la kwanza tangu 2017.

Afisa mmoja wa ngazi ya juu kwenye jeshi la Korea Kusini amesema Jumatatu kwamba meli ya jeshi lake imepata mabaki yanayo amininika kuwa sehemu ya silaha zilizorushwa na Korea kaskazini kwenye bahari karibu na ufukwe wake.