Siku ya Ijumaa, Shirika rasmi la Habari la Korea Kaskazini (KCNA) na gazeti la Rodong Sinmum lilitoa picha kadhaa zikimuonyesha kiongozi Kim Jong Un akitembelea kile ambacho vyombo vya habari vya Kaskazini vimesema ni kituo cha kurutubisha uranium.
Ilikuwa mara ya kwanza kwa Kaskazini kufichua kituo cha kurutubisha uranium hadharani. Katika hotuba ya hivi majuzi ya kuadhimisha miaka 76 toka kuanzishwa kwa serikali yake, Kim amesema Korea Kaskazini, itaongeza maradufu juhudi zake ili kufanya vikosi vyote vya kijeshi vya serikali, pamoja na jeshi la nyuklia, kuwa tayari kikamilifu kwa mapigano.
Wakati huo huo Korea Kaskazini imerusha makombora mengi ya masafa mafupi Jumatano ambayo yalitua baharini katika pwani yake ya mashariki, Korea Kusini na Japan zimesema.
Makombora hayo yalirushwa kutoka Kaechon, kaskazini mwa mji mkuu, Pyongyang, majira ya saa 12:50 asubuhi kwa saa za huko na kuruka kuelekea kaskazini mashariki, Mnadhimu wa jeshi la Korea Kusini amesema bila kutaja idadi ya makombora yaliyofyatuliwa.
“Jeshi letu linaendelea kuwa tayari huku likiimarisha ufuatiliaji na umakini kwa majaribio hayo huku tukisambaza habari kwa haraka kwa Marekani na Japan,” ilisema taarifa.
Takriban dakika 30 baada ya taarifa ya kwanza ya kombora, idara ya ulinzi wa pwani ya Japan, imesema Korea Kaskazini ilirusha kombora lingine na kuanguka.
Komandi ya Indo-Pacific ya Marekani, imesema kupitia mtandao wa X, inafahamu majaribio hayo na imeshauriana na Seoul na Tokyo.