Kongamano ambalo limepangwa na Pakistan kwa ushirikiano na Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kuhamasisha msaada kuisaidia nchi hiyo baada ya kukumbwa na mafuriko makubwa mwaka uliopita, linatarajiwa kufanyika hivi karibuni.
Wajumbe kutoka mataifa 40 wakiwemo marais kadhaa, wawakilishi wa mashirika ya kimataifa ya fedha na wa maendeleo wanatarajiwa kuhudhuria kongamano hilo.
Waziri mkuu wa Pakistan Shehbaz Sharif ataongoza kongamano hilo akishirikiana na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres.
Pakistan inatafuta dola bilioni 16.3 kwa ajili ya kujenga upya na kukarabati mifumo iliyoharibiwa kutokana na mafuriko hayo.
Umoja wa Mataifa umesema kwamba mafuriko ya mwaka 2022 yalisababisha uharibifu mkubwa ambao haujawahi kutokea nchini Pakistan kwa miongo kadhaa.
Watu milioni 33 waliathiriwa na mafuriko hayo, 1,700 kufariki na milioni 8 kukoseshwa makazi.