Kituo kinachofuatilia kesi za virusi vya Corona cha Johns Hopkins cha Marekani kimeripoti mapema Jumapili kwamba kimerekodi maambukizi milioni 224.3 ya COVID-19 ulimwenguni na vifo milioni 4.6 ulimwenguni.
Kituo hicho pia kilisema chanjo bilioni 5.7 zimetolewa. Uingereza inatarajia kutangaza wiki hii mipango yake ya kuwapatia watoto wenye umri wa miaka 12 hadi 15 chanjo dhidi ya virusi vya Corona. Kampeni ya chanjo huenda itaanza baadae mwezi huu.
Wakati huo huo zaidi ya asilimia 50 ya idadi ya watu nchini Japan wamepatiwa chanjo za COVID-19 kulingana na serikali ya Japan. Waziri wa uchumi Yasutoshi Nishimura alisema katika mahojiano kwenye televisheni leo Jumapili kwamba kiwango cha utoaji chanjo kinatarajiwa kufikia asilimia 60 ifikapo mwishoni mwa mwezi Septemba.
Kwingineko, Myanmar inapambana na wimbi la tatu la COVID-19 katika kipindi ambacho mivutano ya kisiasa inaongezeka. Kwa mujibu wa takwimu za shirika la afya Duniani (WHO) zaidi ya watu laki nne wameambukizwa na COVID-19 huko Myanmar na zaidi ya elfu kumi na sita wamekufa.
Maafisa wa afya ya umma nchini humo hata hivyo wanasema wanaamini idadi hiyo iko chini kutokana na uhalisia.