Ushahidi mpya umefichua kwamba aina mpya ya kirusi cha corona cha Omicron tayari kilikuwepo huko ulaya magharibi kabla ya kesi za kwanza kutambuliwa rasmi kusini mwa Afrika.
Maafisa nchini Uholanzi walisema Jumanne kwamba waligundua aina mpya ya kirusi hicho katika sampuli za majaribio mapema Novemba 19 wiki moja kabla ya kugundulika kwa kesi za ugonjwa huo Ijumaa iliyopita miongoni mwa abiria ambao waliwasili huko Amsterdam kwa ndege kutoka Afrika kusini.
Maafisa wa afya nchini Japan na Ufaransa pia walithibitisha kesi zao za kwanza za Omicron leo Jumanne wakijiunga na orodha inayoongezeka ya mataifa yanayoelezea juu ya kirusi hicho ikiwemo Uingereza, Canada, Scotland, Australia, Austria, Uhispania na Sweden.