Kiongozi wa Ukraine aonya vizuizi vya Russia vitasababisha uhaba wa chakula

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy ameonya  Jumamosi kwamba  uvamizi wa Russia nchini kwake utaleta madhara katika utaratibu wa kimataifa na kusababisha hasara kubwa za kiuchumi kwa nchi kadhaa.

Akiongea kupitia mawasiliano ya video na mawaziri na maafisa kutoka nchi 42 wanaohudhuria Kongamano la Shangri-La nchini Singapore, mkutano maarufu wa kiusalama, amesisitiza umuhimu wa hatua madhubuti kuchukuliwa.

“Ninashukuru kwa msaada wenu… lakini msaada huu siyo tu kwa ajili ya Ukraine bali na nyinyi pia,” alisema. “Ni katika uwanja wa mapambano wa Ukraine ndipo kanuni za mustakbali wa dunia hii zinapoamuliwa sambamba na mipaka.”

Rais wa Ukraine akiongea kupitia mawasiliano ya video na mawaziri na maafisa kutoka nchi 42 wanaohudhuria Kongamano la Shangri-La nchini Singapore, mkutano maarufu wa kiusalama.AP Photo/Danial Hakim)

Zelenskyy aliendelea kueleza kuwa nchi kadhaa huko Asia na Afrika zitakabiliwa na njaa na uhaba wa chakula kwa sababu wanajeshi wa Russia wameweka vizuizi kudhibiti usafirishaji wa nafaka kutoka Ukraine, moja ya nchi kuu zinazozalisha chakula duniani.

“Iwapo… Kutokana na vizuizi vya Russia hatuwezi kusafirisha chakula chetu, dunia itakabiliwa na mgogoro mkubwa wa chakula na njaa katika nchi nyingi za Asia na Afrika,” kiongozi huyo wa Ukraine alisema.

Kuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya kupanda kwa bei za bidhaa na hatua za kijeshi za Russia. Russia ilianza kwa kuzuia usafirishaji wa nishati iliyopeleka bei kupanda, na hivi sasa inafanya hivyo hivyo kwa chakula.

Russia imeweka vizuizi katika bandari kwenye bahari za Black Sea na Azov Sea, na kufanya usafirishaji wa chakula cha Ukraine kutofika katika soko la dunia. Hilo linaumiza dunia nzima siyo tu waukraine, Zelenskyy alisema.