Kiongozi wa Hamas ashitakiwa Marekani

Wizara ya Sheria ya Marekani, Jumanne imetangaza mashtaka ya jinai dhidi ya kiongozi wa Hamas, Yahya Sinwar na wanamgambo wengine wakihusishwa na shambulizi la Oktoba 7, 2023 nchini Israel.

Mashitaka ya jinai yaliyowasilishwa katika mahakama ya serikali kuu jijini New York yanajumuisha mashtaka ya kula njama ya kutoa msaada wa mali kwa shirika la kigeni la kigaidi, na kusababisha vifo.

“Mashtaka ambayo hayajafungwa ni sehemu moja tu ya juhudi za kulenga kila kipengele cha operesheni za Hamas,” Mwanasheria Mkuu Merrick Garland, amesema katika taarifa yake ya video.

Sinwar aliteuliwa kuwa mkuu wa jumla wa Hamas baada ya mauaji ya Ismail Haniyeh nchini Iran na yupo katika orodha ya wanaotafutwa zaidi na Israeli.

Anaaminika kuwa alitumia muda mwingi wa miezi 10 iliyopita akiishi kwa kujificha Gaza, na haijulikani ni kiasi gani ana mawasiliano na dunia ya nje.