Helene chasababisha uharibifu mkubwa Kusini Mashariki mwa Marekani

  • VOA News

Baadhi ya nyumba zilizoharibiwa na kimbunga Helene kwenye jimbo la Florida

Majimbo ya  kusini mashariki mwa Marekani yanaendelea kukabiliana na vifo pamoja na ukosefu wa vifaa muhimu kwenye maeneo ya ndani, huku nyumba zikiharibiwa kutokana na kimbunga Helene, ambacho maafisa wamesema kitakuwa na athari kubwa.

Gavana wa North Carolina, Roy Cooper, amesema Jumapili kwamba idadi ya vifo kwenye jimbo hilo imefika 11, wakati ikitarajiwa kuongezeka, huku timu za uokozi zikijitahidi kufikia maeneo ya ndani, yaliyokumbwa na mafuriko pamoja na kuharibika kwa miundo mbinu kama barabara.

Jimboni Florida na hasa kwenye kaunti ya Big Bend, wakazi wameripotiwa kupoteza karibu kila kitu, huku asilimia 97 wakiwa hawana umeme kutokana na kimbunga hicho.

Rais wa Marekani Joe Biden Jumamosi alisema kuwa uharibifu wa Helen umekuwa mkubwa huku akiahidi msaada wa serikali kuu kwenye majimbo yaliyoathiriwa. Helen ni kimbunga cha 8 kutoka bahari ya Atlantic kupiga Marekani kwenye msimu huu wa vimbunga ulioanza Juni .