Kim aahidi kufunga eneo la kujaribia silaha za nyuklia

Rais wa Korea Kusini Moon Jae-in (kulia) na Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un

Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un ameahidi kufunga eneo la kujaribia silaha za nyuklia nchini humo ifikapo Mei na kuwashirikisha katika mchakato huo waandishi wa habari na wataalamu kutoka Korea Kaskazini na Marekani, Ofisi ya Rais ilioko Seoul imetoa tamko hili Jumapili.

Korea Kusini imeeleza kuwa mafanikio hayo yamepatikana baada ya kufanyika mkutano wa kihistoria wa siku ya Ijumaa kati ya viongozi wa nchi hizo mbili.

Kim ametoa maoni hayo wakati wa mkutano wake na Rais wa Korea Kusini Moon Jae-in Ijumaa katika Kijiji kilichopo mpakani, ambapo pia alieleza kuwa anamatumaini kutakuwepo mkutano ambao unatarajiwa kufanyika baina yake na Donald Trump, akisema rais wa Marekani atafahamu karibuni kuwa yeye “sio mtu ambaye” angepiga makombora kuilenga Marekani, Msemaji wa Moon Yoon Young-chan amesema.

Moon na Kim wakati wa mkutano wao huo waliahidi kushirikiana kufikia “ utokomezaji kamili wa silaha za nyuklia” zilizoko katika Rasi ya Korea, lakini walikuwa hawakueleza jinsi watakavyo hakiki au ratiba ya utekelezaji huo.

Kadhalika Seoul ilikuwa imeendelea kuwasiliana na Pyongyang na Washington ili kuandaa kuwepo mkutano huo kati ya Kim na Trump, ambao unatarajiwa kufanyika mwezi ujao au mapema Juni.

Kim pia amesema kuwa yuko tayari kufanya mazungumzo ya kurejesha uhusiano na Japan, Korea Kusini imesema.

Rais Moon amemfahamisha Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe Ijumaa juu ya mkutano wa Ijumaa alioufanya na Kim.

Moon amemwambia Abe kuwa alifikisha ujumbe wa Japan juu ya azma yake ya kurejesha mahusiano na Korea Kaskazini baada ya nchi hizo mbili kukubaliana mambo “yaliyopita katika historia.”

Ofisi ya Moon imesema kuwa Kim alijibu kuwa yeye yuko tayari kufanya mazungumzo na Japan.

Ofisi hiyo haikutoa maelezo zaidi kuhusu hilo lakini Abe ameripotiwa akisema kuwa Moon katika mkutano wake na Kim alizungumzia kitendo cha Korea Kaskazini kuwateka raia wa Japan.