Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania atafanya historia wiki ijayo kwa kuyahutubia mabaraza mawili ya bunge la Kenya kabla ya kustaafu na kabla ya uchaguzi mkuu nchini Tanzania.
Hili litakuwa ni tukio la kihistoria nchini Kenya kwa kiongozi wa taifa la kigeni ambaye yungali kwenye uongozi kuyahutubia mabaraza mawili ya bunge la Kenya-yaani Bunge la Wawakilishi na Baraza la Senate.
Your browser doesn’t support HTML5
Kulingana na Spika wa Bunge la Wawakilishi Justin Muturi, Rais Kikwete atayahutubia mabaraza hayo mawili siku ya Jumanne, Oktoba 6. Atakuwa kwenye ziara rasmi nchini Kenya wakati wa hotuba hiyo.
Tayari Spika wa Bunge Justin Muturi na Spika wa Baraza la Senate Ekwee Ethuro wameidhinisha hotuba hiyo kuambatana na Katiba ya Taifa. Anasema walikuwa wamepokea ombi hilo kutoka kwa afisi ya Rais Kenyatta kumuwezesha Rais Kikwete kuyahutubia mabunge hayo mawili.
Kiongozi wa kwanza kuyahutubia mabaraza hayo mawili ni aliyekuwa Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan wakati wa ziara yake nchini Kenya na kabla ya kushindwa katika uchaguzi nchini mwake.
Wachunguzi wa kisiasa Nairobi wanahisi huenda Rais Kikwete akazungumzia maswala yanayohusu ushirikiano kati ya Kenya na Tanzania pamoja na maswala nyeti yanayokumba jumuiya ya Afrika Mashariki, kwa mfano hati za kusafiria, kodi na ushuru kwa bidhaa kutoka nchi moja kwenda nyingine mwanachama pamoja na ndoto ya shirikisho la kisiasa la jumuiya ya Afrika Mashariki. Imeripotiwa na Mwai Gikonyo, Nairobi.