Waendesha mashtaka nchini Kenya wamesema Jumatatu kuwa wamemsafirisha mwanamme anayetuhumiwa kumuua mpenzi wake nchini Marekani katika kesi ambayo iligonga vichwa vya habari baada ya kutoroka mikononi mwa polisi mjini Nairobi.
Kevin Kang'ethe alikuwa akisakwa kimataifa kwa miezi mitatu baada ya kutoroka Marekani na kukimbilia katika nchi yake ya asili Kenya kufuatia mauaji ya Margaret Mbitu, ambaye alikutwa amechomwa visu hadi kufa katika eneo la kuegesha magari katika uwanja wa ndege wa Logan huko Boston mwezi Novemba.
Alikamatwa nchini Kenya mwezi Januari, lakini baada ya wiki moja tu akiwa kizuizini, Kang'ethe alitoroka kutoka kwenye jela alikokuwa akishikiliwa, na kupelekea aibu kubwa kwa idara ya polisi Kenya. Alikamatwa tena mwezi Februari mahala alipojificha katika nyumba ya jamaa yake, nje kidogo ya jiji la Nairobi.
Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) nchini Kenya ilisema katika taarifa kwamba Kang'ethe alisafirishwa kutoka Kenya siku ya Jumapili na atakabiliwa na mashtaka ya mauaji katika mahakama moja huko Boston nchini Marekani kesho Jumanne.
Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, Renson Ingonga alikuwa amemhakikishia mkurugenzi wa FBI nchini Marekani, Christopher Wray, wakati wa mazungumzo jijini Nairobi mwezi Juni kwamba afisi yake ilikuwa “imejipanga kuhakikisha haki inayohusisha kesi hii inatendeka kwa haraka”, ilisema taarifa hiyo.