Kesi za katazo la wasafiri zaanza kusikilizwa Jumatano

Maandamano ya kupinga amri ya kiutendaji mpya.

Mawakili walioko katika kikundi kinacho shughulikia kesi zinazotaka amri ya Donald Trump iliokataza wasafiri na wakimbizi kuingia Marekani izuiliwe, wanasema wanasubiri maamuzi ya kesi za mahakama za rufaa zilizopangwa kusikilizwa Jumatano.

Kesi hizo zitasikilizwa huko Maryland, Hawaii na Washington State na mawakili wako tayari kukabiliana na maamuzi yoyote ambayo yanaweza kuleta athari katika utekelezaji huo Alhamisi unaohusu amri za katazo la kusafiri zilizotolewa karibuni.

Majaji watatu wa mahakama za rufaa mwezi uliopita waliendeleza maamuzi ya Jimbo la Washington yaliyo simamisha amri ya katazo la kusafiri, lililotolewa Januari 27, wiki moja baada ya kuapishwa Trump. Rekebisho la amri lililotolewa wiki iliyopita, lilijaribu kukuwepa kesi zilizofunguliwa, shinikizo la upinzani na maudhi yaliyo sababishwa na amri ya kwanza.

Amri ya kiutendaji ya hivi karibuni kabisa inayo husiana na kusafiri, alioitoa Trump March 6, imekataza kupewa viza raia wa Iran, Libya, Somalia, Sudan, Syria na Yemen kwa siku 90 na kuweka katazo lakuingia kwa wakimbizi kwa siku 120, kuanzia Machi 16, na serikali ikinasibisha hilo na tatizo la “usalama wa taifa.”

Wapinzani wa amri hiyo- ambayo itaathiri nchi sita zenye Waislamu wengi na idadi kubwa ya wakimbizi ambao wanasubiri kupatiwa makazi wakiwemo Waislamu wengi- wameendelea kusema kuwa amri ya pili iliyotolewa ni ya ubaguzi wa kidini na kinyume cha katiba na wanampango wa kuendelea kutumia mkondo wa sheria kupinga sera za rais.

“Hata kama Rais Trump atajaribu kukanusha kauli aliyoitoa hapo awali kwamba hili katazo la kusafiri liliwalenga Waisalmu na lilikuwa linawabagua Waislamu, bado hatoweza kufuta amri hii ilipotokea—katika juhudi za kuwabagua Waislamu kwa msingi wa dini yao,” amesema Cecillia Wang, Naibu Mkurugenzi wa Sheria wa Umoja wa Haki za Kiraia wa Marekani wakati akizungumza na waandishi Jumanne..

Katika nyakati tofauti wakati akifanya kampeni ya urais, Trump ametoa kauli za jumla zinazotaka wakimbizi na waislamu wazuiliwe kuingia Marekani. White House imeendelea kukanusha kwamba amri hiyo inawalenga Waislamu.

Kwa sababu ya notisi ya siku 10 iliyotolewa, ambayo haitekelezwi mara moja, mtafaruki uliowachanganya watu katika viwanja vya ndege hautarajiwi kuwepo hapo amri itapoanza kutumika siku ya Alhamisi.

Mark Doss, wakili anayefanya kazi na Mradi wa Kuwasaidia Wakimbizi wa Kimataifa, amesema mawakili watakuwa tayari kukabiliana na amri hiyo katika viwanja vya ndege Alhamisi “iwapo kutakuwa na matatizo yoyote.”