Kusikilizwa kwa kesi ya kiserikali dhidi ya wamarekani watatu wenye asili ya kisomali wanaoshukiwa kutoa misaada kwa kundi la Islamic State imeanza Jumatatu katika jimbo la Minnesota.
Mohamed Farah, mwenye umri wa miaka 22, Guled Omar, mwenye umri wa miaka 21, na Abdirahman Daud, mwenye umri wa miaka 22, ni miongoni mwa wanaume kadhaa kutoka Minnesota waliokutana mara kadhaa kati ya Machi 2014 na Aprili 2015 kujadili njia muafaka ya kusafiri kwenda Syria kwa nia ya kujiunga na Islamic State.
Wote walisimamishwa na maafisa wa usalama kabla ya kuingia ndani ya ndege. Waendesha mashitaka wa Serikali wamesema kuwa wote walipanga njama ya kutekeleza mauaji nje ya Marekani na iwapo watapatikana na hatia, huenda wakapewa kifungo cha maisha. Hata hivyo wote wamekana mashitaka hayo.