Mahakama ya juu ya Umoja wa Mataifa itasikiliza shauri la Afrika Kusini, na Israel, wiki ijayo baada ya Pretoria kufungua kesi kwa kile ilichokiita mauaji ya kimbari ya Israel huko Gaza.
Afrika Kusini inaitaka Mahakama ya Kimataifa ya Haki kuamuru kwa haraka Israel kusitisha operesheni zake za kijeshi za Gaza, katika kesi ambayo Israel ilipingwa huku ikikasirishwa.
Marekani, Jumatano iliikosoa Afrika Kusini, kwa kuwasilisha kesi ya mauaji ya kimbari, na kupinga shutuma dhidi ya Israel kuhusu vita vyake huko Gaza.
“Uwasilishwaji huu hauna maana, hauna tija na hauna msingi wowote,” msemaji wa Baraza la Usalama wa taifa, John Kirby aliuambia mkutano na wanahabari.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, Matthew Miller amesema kwamba kutokana na tathmini ya Marekani, “hatujaona vitendo vinavyojumuisha mauaji ya kimbari kwa wakati huu.”