Kenyatta, Odinga wafanya mazungumzo

Rais Uhuru Kenyatta, na kiongozi wa upinzani Raila Odinga

Rais wa Kenya na kiongozi wa upinzani nchini Kenya kwa pamoja wameahidi kuanza mchakato wa kutafuta suluhu baada ya uchaguzi uliokuwa na ushindani mkali.

Uhuru Kenyatta na Raila Odinga walizungumza kupitia televisheni ya taifa baada ya mkutano wao wa kwanza wa hadhara tangia kufanyika uchaguzi.

Takriban watu 150 waliuwawa kutokana na madhara ya uchaguzi uliokuwa unapingwa.

Mapema mwaka 2018, Odinga alijiapisha kama “rais wa wananchi” na kukataa kumtambua Kenyatta kama Rais baada ya kushinda uchaguzi.

Mpaka kufikia hivi sasa, pande zote zilikuwa zimekataa wito wa kufanya mazungumzo.

Katika hotuba ya pamoja, Rais Kenyatta alimtambulisha Odinga kama “kaka yake.”

Kenyatta amesema: “Tutaanza na mchakato wa mazungumzo juu ya kile kinachotusumbua na kile kinachotugawanya.”

Odinga amesema kuwa ni “wakati wa kuondosha tofauti zetu”.