Kenya inaonekana kulipa uzito suala la kujitoa katika Mahakama ya Kimataifa ya ICC. Katika hotuba yake Jumatatu kwenye sherehe za uhuru wa Kenya, rais wa nchi hiyo alitoa ishara ya wazi kuwa wako katika harakati za kujitoa kwenye mahakama hiyo.
Rais Uhuru Kenyatta amesema serikali yake inatathmini hoja mbili ambazo zimepitishwa na Bunge la Kenya juu ya kujitoa katika mahakama hiyo.
Alisema uamuzi huo ulichochewa kutokana na mahakama ya ICC kushindwa kufanya mabadiliko kwa kuheshimu utaifa wa nchi ambazo ni wanachama.
“Uamuzi wetu wa kuchagua ndio msingi wa namna gani tutaendesha nchi zetu kufikia malengo yake kama taifa huru,” Kenyatta alisema.
“Muasisi wetu alipambana kwa ushujaa kupata haki ya kufanya maamuzi bila ya kuingiliwa na ushawishi wa nje. Leo hii dunia imegubikwa na vita vyenye azma na utashi wa kunyonya rasilimali za mataifa huru."
Kenyatta amesema kuwa ICC ilionyesha upendeleo wakati walipo kuwa wanashughulikia suala la Kenya na nchi nyingine za kiafrika tayari zimetambua udhaifu huo.
Amesema Kenya imekuwa mstari wa mbele kuunga mkono taasisi za kimataifa ambazo zimefuata uadilifu na kuheshimu uhuru wa taifa kama ni sehemu ya kuendeleza uthabiti duniani.
“Kesi za wakenya katika Mahakama ya ICC zimemalizika, lakini uzoefu tulioupata umetupa sababu za kuona kuwa taasisi hii imekuwa ni chombo cha siasa za ubabe duniani na sio tena taasisi iliyojengwa katika kutoa haki,” alisema Kenyatta.