Kenyatta aiambia CNN haki za mashoga sio tatizo Kenya

Rais Uhuru Kenyatta

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya amesisitiza kuwa haki za mashoga zina umuhimu mdogo kwa wananchi wa Kenya.

Katika mahojiano na Shirika la televisheni ya Marekani CNN yaliopeperushwa siku ya Ijumaa usiku, Uhuru amesema kuwa suala hilo halina mjadala na linakwenda kinyume na imani za Wakenya waliowengi.

“Nataka niweke wazi, sitojihusisha na suala ambalo halina umuhimu mkubwa kwa wananchi wa Kenya. Hili siyo suala la haki za binadamu, hili ni suala la kijamii, lakini ni misingi tu ya utamaduni kama watu bila ya kujali unatokea katika jamii gani.

Rais alisema: “Wao pia lazima watambue kuwa uhuru wao lazima uheshimu maadili ya jamii ambayo wanaishi ndani yake kwa sababu hili sio suala la serikali kukubali au kukataa. Hili ni suala la kijamii.”

Rais amesema kuwa sheria za Kenya zinaweka wazi kuwa ushoga ni kinyume cha sheria na Wakenya waliowengi wanakubaliana na hilo.

“Hizo ni sheria tulizokuwa nazo na ni sheria zinazoungwa mkono kwa asilimia 100 na asilimia 99 ya Wakenya bila ya kujali wanatokea wapi,” amesema.

Hii ni mara ya pili Uhuru anazuia mjadala juu ya haki za mashoga baada ya kutupilia mbali wito wa Barrack Obama ukiitaka serikali yake kuwakubali makundi mbalimbali ya mashoga mnamo mwaka 2015.

“Ipo haja ya kuwa wawazi katika kujadili baadhi ya masuala haya. Wakenya na Wamarekani yako maadili ambayo wanashirikiana kama vile demokrasia, ujasiriamali na maadili ya familia lakini baadhi ya vitu siyo sehemu ya dini na utamaduni wetu, na hatuwezi kulazimisha wananchi wetu mambo ambayo hawayapendi,” amesema Uhuru.

Lakini Uhuru amesema kuwa yeye ni muumini wa misingi ya kuwatendea watu haki kwa kufuata sheria.

Alipoulizwa kuhusu vurugu zilizotokea baada ya uchaguzi wa Kenya 2017, Uhuru alikanusha kuwa alihusika katika hilo na kusema serikali yake hakuendesha vurugu hizo.

Alisema kuwa hakuna mtu anaefurahia vifo vya namna yoyote. Ni wazi kabisa kuwa kulikuwa na hali za kusikitisha na baadhi ya matukio hayo yalikuwa yamechochewa na baadhi ya watu kwa maslahi ya kisiasa.

“Ikiwa nitafanya tathmini juu ya matatizo yaliyotokea, Kenya imepita katika matatizo tuliyoyaona mwaka 2010 ambapo ilikuwa ni vita tupu. Ni wajibu wetu kukua kimawazo hadi tufikie kiwango cha kuwa lazima tukubali siasa za ushindani kuwa siyo uadui,” hilo ni muhimu sana amesema.

Uhuru ameiambia CNN kuwa wale walioathiriwa na vurugu hizo ni lazima wawasilishe madai yao ili kupata haki zao. Lakini hakutoa muda maalum wa jinsi mipango hiyo itakavyo tekelezwa.

“Kama mzazi , ninasikitiko juu ya watu hao walioathiriwa na vurugu, na nataka niwahakikishie nitafanya kila niwezalo kuhakikisha jambo kama hili halitokei tena na kuweka utaratibu wote wazi kuhakikisha yoyote aliyepoteza maisha au mali anaweza kupata haki yake,” ameahidi.

Alipobanwa juu ya kero iliyokuwa imeenea juu ya kufungwa kwa vyombo vya habari jambo ambalo lilifuatia kujiapisha kwa Raila Odinga, Uhuru alisema lilikuwa kosa la vyombo hivyo, na kuwa walivunja sheria.

Kenya ni nchi yenye vyombo vya habari vinavyoripoti zaidi ya 70 ikiwemo CNN. Lakini ni vyombo vitatu tu vilivyo fungiwa na hili lilikuwa baada ya mjadala mrefu na vyombo hivyo kabla ya kufikia uamuzi wa kuvifungia, na sote tulikubaliana na watu wa sheria kwamba kile walichokuwa wanataka kukipeperusha kinapelekea kosa la uhaini,” amesema Uhuru.