Akizungumza katika shule ya msingi ya Mutomo iliyoko kwenye eneo la uwakilishi la Gatundu South, Kenyatta alisema yuko tayari kulinganisha taifa baada ya uchaguzi ulioleta mgawanyiko mkubwa.
Rais huyo alikuwa akijibu maswali ya waandishi wa habari muda mfupi baada ya kupiga kura.
Kenyatta aidha alieleza masikitiko yake kwamba zoezi la upigaji kura halikufanyika katika baadhi ya maeneo ya nchi kwa sababu za kiusalama.
"Nimepata ripoti kwamba IEBC inalishughulikia suala hilo japokuwa sijapata maelezo ya kutosha. Ni haki ya kila Mkenya kupiga au kutopiga kura kwa amani,' alisema Kenyatta.
Alipoulizwa iwapo ana matumaini ya ushindi wa kishindo pamoja na kuwa baadhi ya wapiga kura wamesusia zoezi hilo, Uhuru alisema: "Bila shaka ni matumaini ya mgombea yeyote kwamba atashinda.'
Rais huyo alikariri kauli yake ya siku ya Jumatano kwamba hatua ya kubatilishwa kwa uchaguzi wa urais na mahakama ya juu ni ishara tosha kwamba Kenya imepiga hatua kubwa kidemokrasia.
Uchaguzi wa Alhamisi ulioendelea katika maeneo mengi lakini baadhi ya kaunti ziliripoti ghasia na maafisa wa IEBC na vifaa vyao kutoweza kufika kwenye vituo vya kupigia kura.
Afisa mmoja wa polisi alijeruhiwa katika neo la Kibera kufuatia makabiliano kati ya walinda usalama na watu wanaoaminika kuwa wafuasi wa muungano wa upinzani, NASA, ambao umetangaza kubadilishwa kwa jina lake na kuwa vuguvugu la ukombozi.
Odinga alitangaza kwamba hatashiriki katika uchaguzi huo wa marudio.