Kenya na Marekani zatofautiana kuhusu Al-Shabaab

Wanamgambo wa Al-Shabaab.

Mkutano wa siku mbili wa Ujasusi na Usalama ulikamilika jijini Nairobi nchini Kenya Jumanne wakati ambapo Kenya imeinyoshea kidole Marekani kwa kusita kuunga mkono juhudi zake za kutaka kundi la wanamgambo wa Al-shabaab  kuorodhesha kama kundi la Kigaidi.

Wakati huo huo, Balozi wa Marekani nchini humo Kyle McCarter amepuuzilia mbali kauli hiyo na kukariri kuwa Marekani imeunga juhudi zote za kulilemaza kundi hilo lililo na makao yake nchini Somalia.

Wabunge wa Kenya ni miongoni mwa wajumbe zaidi ya 250 kutoka nchi kama vile Ufaransa, Marekani, Uingereza, Nigeria, Brazil, Mexico, Italia, Ethiopia, Argentina, Columbia, Zambia, Zimbabwe, Djibouti na Ujerumani waliokutana jijini Nairobi kujadili mkakati wa kushirikiana na asasi husika za serikali za kimataifa kubuni sheria na sera za kupambana na uhalifu, hususan ugaidi.

Watalaamu hao, wanaojumuisha wanasiasa pia walijadili umuhimu kwa kushirikiana kufahamishana maelezo ya kijasusi kulemaza uhalifu wa kimtandao, ulanguzi wa dawa za kulevya, ufisadi, uchakatishaji wa fedha miongoni mwa aina nyingine za uhalifu.

Mkutano huuo unajiri wiki chache baada ya baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupinga pendekezo la serikali ya Kenya kutaka kundi la wanamgambo wa Al-Shabaab kujumuishwa miongoni mwa makundi ya ulimwengu ya kigaidi yaliowekewa vikwazo vya kimataifa.

Wanaharakati wa haki za kibinadamu waliwasilisha nyaraka za maelezo mbele ya baraza la umoja huo wakisema kuwa iwapo hatua ya Kenya itakubalika basi huenda raia wa Somalia wanaoishi katika himaya ya Al-Shabaab wakashindwa kupata misaada ya kibinadamu.

Lakini Kenya tayari imeeleza kutoridhishwa na hatua ya baraza hilo la usalama la umoja wa Mataifa na ni kauli ambayo Spika wa bunge la Kenya, Justin Muturi, ameirejelea wakati huu akiilaumu serikali ya Marekani kwa kusitasita katika kulitangaza kundi hilo la wapiganaji wa Al-Shabaab kuwa la kigaidi.

Muturi alisisitiza kuwa hatua hiyo inalipa kundi hilo mwanya wa kufikia usaidizi wa kifedha kutoka kwa mashirika mbalimbali, hali itakayokuwa pigo kwa juhudi za kulilemaza maana litaonekana kuwa kundi la kijamii nchini Somalia.

Hata hivyo, balozi wa Marekani nchini Kenya Kyle McCater alipuuzilia mbali madai hayo na kusisitiza kuwa Marekani imekuwa mstari wa mbele kulemaza uwezo wa kundi hilo, hususan baada ya kuunga mkono azimio nambari 751 la Umoja wa Mataifa kulioriodhesha kundi lhilo kuwa la kigaidi ambalo linafaa kukabiliwa vilivyo na jamii ya kimataifa.

Balozi Martin Kimani ambaye ni mkurugenzi wa idara ya taifa la Kenya ya kukabiliana ugaidi aliiambia Sauti ya Amerika kuwa hatua ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa inatia doa juhudi za kupambana na ugaidi ulimwenguni, hatua ambayo hairidhishi kamwe.

Aidha, Mbunge wa Kenya, Didmus Baraza, alikariri kuwa bunge la nchi hiyo litaendelea kuvitengea vitengo vya Kenya vya kupambana na ugaidi fedha nyingi na hivyo basi hawatafedheheshwa na hatua ya Umoja wa Mataifa.

-Imetayarishwa na mwandishi wa Sauti ya Amerika, Kennedy Wandera, akiwa Nairobi, Kenya.