Kenya: zaidi ya waumini 100 wa dhehebu walifariki kutokana na njaa, uchunguzi wa kitaalamu wathibitisha

Waziri wa mambo ya ndani wa Kenya Kithure Kindiki, akikagua makaburi ambako waumini wa dhehebu la Kikristu wamezikwa, katika kitongoji cha mji wa Malindi, Aprili 25, 2023

Uchunguzi wa kwanza wa kitaalamu kwenye maiti zilizogunduliwa katika makaburi yanayohusishwa na mchungaji wa Kenya anayeshukiwa kuwahimiza waumini kujinyima chakula hadi kufa, ulithibitisha njaa kama sababu ya vifo hivyo, maafisa wamesema Jumatatu.

Wataalam waliofanya uchunguzi wa kwanza kwenye zaidi ya miili 100 iliyofukuliwa katika msitu wa pwani waliwachunguza watoto tisa wenye umri wa mwaka mmoja hadi 10 pamoja na mwanamke mmoja.

“Wengi wao walikuwa na ishara za njaa,” mtaalamu mkuu wa serikali Johansen Oduor alisema baada ya uchunguzi wa maiti kufanyika katika chumba cha kuhifadhi maiti katika mji wa Malindi.

“Tuliona ishara za watu ambao hawajala, hakukuwa chakula tumboni, kiwango cha mafuta mwilini kilikuwa kidogo,” alisema.

Lakini Oduor aliongeza “Kutokana na kile tunachosikia, kulikuwa na dalili kwamba walikufa kwa kufunikwa mapua na vinywa vyao, hiyo inaweza kuwa sababu ya kukosa hewa. Hilo lilionekana kwa watoto wawili.”

Katika kisa hicho ambacho kilizuka mwezi uliopita, na kulishangaza taifa hilo lenye imani kubwa ya kidini, kiongozi wa dhehebu Paul Mackenzie Nthenge anashtumiwa kuwashawishi wafuasi wake kufika kwa Mungu kwa kujinyima chakula.