Kenya yazima jaribio la shambulizi la kigaidi - polisi

Kenya ilitangaza Jumapili kwamba ilizima jaribio la mashambulizi ya kigaidi na kuwakamata washukiwa sita wanaoaminika kuwa na uhusiano na kundi la Al-Shabaab.

Maafisa wa usalama nchini Kenya, wamewakamata wanaume sita wanaoshukiwa kuwa na uhusiano na wanamgambo wa Al-Shabaab na wanaotuhumiwa kwamba walikuwa wakipanga njama ya kufanya mashambulizi nchini humo.

Shirika la habari la Reuters liliriipoti kuwa Inspekta mkuu wa polisi wa Kenya, Joseph Boinnet alisema Jumapili kwamba wawili kati ya washukiwa hao ni raia wa Kenya,na hao wengine ni raia wa Somalia.

Aidha polisi walisema walinasa vifaa vilivyokusudiwa kutumika katika kutekeleza mashambulizi, vikiwa ni pamoja na vilipuzi, na vifaa vya kutengeneza mabomu, kama vile kemikali ya TNT.

Boinnet alisema kwamba watu hao walikuwa wametumwa na makamanda wao kutoka eneo la Burhanche, nchini Somalia, ili kutekeleza mashambulizi nchini Kenya.

Alisema maafisa wa usalama wa Kenya walishirikiana na wenzao nchini Somalia ili kuwakamata washukiwa hao.

Kenya imekuwa ikikabiliwa na changamoto za kiusalama za mara kwa mara tangu ilipotuma vikosi vyake nchini Somalia mnamo mwaka wa 2011.

Katika siku za hivi karibuni, nchi hiyo imepoteza maafisa 20 wa kulinda usalama kufuatia mashambulizi kadhaa hususan kwenye vilipuzi vya kujitengenezea viliyotegwa kwenye barabara za eneo la Kaskazini mwa nchi, karibu na mpaka wake na Somalia.