Kenya yasema haina fedha

Waziri wa Fedha Henry Rotich (kushoto)

Waziri wa Fedha wa Kenya Henry Rotich amesema kuwa serikali inakabiliwa na matatizo kadhaa katika kufadhili baadhi ya miradi yake ya maendeleo.

Rotich ameweka bayana pendekezo la kupunguza matumizi ya mabilioni ya fedha zilizokuwa zimetengwa kwa kaunti kadhaa ambazo ni kati ya shilingi bilioni 15 na shilingi bilioni 17.

Wakati akiongea mbele ya kamati ya fedha na bajeti ya Baraza la Seneti Jumatano, Rotich amesema hali hiyo inatokana na mamlaka ya mapato Kenya kushindwa kukusanya kodi kwa kufikia malengo waliopewa katika makadirio ya ukusanyaji wa kodi yaliyopitishwa.

“Tumezungumza na KRA juu ya njia bora ya kufikia udhibiti wa ukusanyaji kodi kamili kwa pato la ndani ya nchi na pato la bidhaa zinazoingia nchini,” Rotich ameiambia kamati hiyo inayoongozwa na Seneta wa Mandera Mohamed Maalim Mahamud.

Waziri ameongeza kuwa; “tunahitaji kulizungumzia suala hili pamoja (maseneta) na magavana kwamba kiwango cha mapato tunachojadili siyo rahisi kukusanya kutokana na changamoto nilizozielezea.”

Katika mwaka wa fedha 2018, shilingi bilioni 302 zilikuwa zimetengwa kwa kaunti za serikali 47 katika uwiano uliosawa wa mapato yaliyokusanywa, ikimaanisha kuwa katika hali mbaya kabisa ya kiuchumi, mgawanyo huo ungeweza kupungua kufikia shilingi bilioni 285.

Kwa mujibu wa waziri wa fedha, upungufu huo wa ukusanyaji mapato kama ulivyokuwa umekadiriwa mwezi Machi 2017 wakati bajeti hiyo iliposomwa mapema mwaka 2017 ili kuwezesha uchaguzi mkuu kufanyika Agosti 8, umesababishwa na kipindi kirefu cha kuandaa uchaguzi na ukame uliokuwa unaikabili Kenya.

Waziri anasema kuwa hili liliathiri ukusanyaji wa mapato kwani ilizorotesha shughuli za biashara nchini.