Kenya yaondoa kanuni za Covid-19

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta

Kenya Ijumaa imetangaza kuondoa kanuni zote zilizowekwa kutokana na janga la corona zikiwemo kuzuia mikusanyiko ya watu ndani ya majengo kama vile nyumba za ibada pamoja na wasafiri wa ndege kuonyesha vibali vya kupimwa mara baada ya kutua nchini.

Kwa mujibu wa shirika la habari la reuters, wakenya hata hivyo watahitajika kuheshimu kanuni za kiafya kama kunawa mikono pamoja na kuweka umbali unaohitajika, wakati ikiwa sio lazima kuvaa barakoa tena kwenye maeneo ya umma.

Waziri wa afya Mutahi Kagwe wakati akihutubia wanahabari pia amesema kwamba kanuni za karantini kwa watu walioambukizwa pia zimeondolewa mara moja. Ameongeza kusema kwamba idadi ya maambukizi katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita imekuwa chini ya asilimia 1, na kwamba huenda hali hiyo ni kutokana na idadi kubwa ya wakenya waliopokea chanjo.

Novemba mwaka jana serikali ilitangaza kwamba watu wangehitajika kuonyesha udhibitisho wa chanjo kufikia Decemba 21, ili kupata huduma muhimu kwenye mashule, migahawa, bar,ofisi za serikali pamoja na mbuga za wanyama miongoni mwa sehemu nyingine.