Kenya yaelezea mikakati ya kiusalama wakati wa uchaguzi

Msemaji wa serikali ya Kenya, Eric Kiraithe.

Msemaji wa serikali ya Kenya Eric Kiraithe, Jumatano aliwahakikishia wapiga kura kwamba serikali imeweka mikakati ya kutosha ya wanalinda Wakenya wote mnamo siku ya uchaguzi na hata baada ya zoezi hilo litakalofanyika siku ya Jumanne.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa KICC jijini Nairobi, Kiraithe alisema kwamba kumekuwa na visa vingi vya uenezaji wa habari za kupotosha na kuwashutumu viongozi wa kisiasa wakiwa ni pamoja na mgombea mwenza wa muungano wa upinzani wa NASA, Kalonzo Musyoka, na seneta wa Kisumu mjini, Anyang’ nyong’o, ambao amesema wametoa taarifa za kutowajibika kama viongozi wa kisiasa.

Aidha alimtaka mbunge wa Jubilee, Moses Kuria, kuwajibika katika matumizi yake ya mitandao ya kijamii. Kuria alikua ameandika ujumbe wa kumdhalilisha aliyekuwa naibu mkurugenzi wa kitengo cha teknolojia na mawasiliano kwenye tume ya IEBC, Chris Msando, ambaye mwili wake ulipatikana msituni siku ya Jumatatu.

Kiraithe alisema maafisa wa kulinda usalama wanaendelea kupata mafunzo ya pamoja ya jinsi ya kuhakikisha kuna usalama nchini katika kipindi hiki cha uchaguzi na hata baadaye.

"Ninataka kuthibitisha kwamba mafunzo hayo ya pamoja yanaendelea ili kuwatayarishisha maafisa hao kwa zoezi la uchaguzi. Polisi watakuwa kwenye vituo vya kupigia kura kuwaunga mkono maafisa wa IEBC, kuzuia uhalifu na kuhakikisha sharia inalindwa," alisema afisa huyo.

Alivitaka vyombo vya habari kuonyesha uwajibikaji na kuongeza kwamba wale wanaotumia mitandao ya kijamii kueneza propaganda au uvumi watachukuliwa hatua kali za kisheria hata baada ya uchaguzi wa Jumanne.

Aidha serikali ilieleza kwamba itatekeleza wajibu wake kulingana na kanuni za tume huru ya uchaguzi na mipaka, na kuwataka wapiga kura kuondoka kwenye vituo vya kupigia kura punde tu baada ya kumaliza shughuli zao, ili kuwapa nafasi Wakenya Wengine, na kuzuia uwezekano wa utovu wa nidhamu.

Haya yalijiri siku moja tu baada ya waziri wa ulinzi wa Kenya, Rachelle Omamo, kuwahakikishia wananchi kwamba serikali haina mipango ya kutumia jeshi katika uchaguzi wa mwaka huu.

Upinzani, ukiongozwa na mgombea wa muungano wa NASA, Raila Odinga, ulikuwa umeelezea wasiwasi kwamba jeshi lingetumika, na kutoa nyaraka za mawasiliano ambazo ulisema, zilikuwa zimetoka kwa wanajeshi waandamizi kama matayarisho ya kuingilia kati uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Upinzani ulidai kwamba serikali ilikuwa na nia ya kuwatia hofu wapiga kura hususan katika maeneo yanayoaminika kuwa ngome za upinzani.

Na pamoja na kauli hiyo ya waziri wa ulinzi, rais Uhuru Kenyatta alisema viongozi wa upinzani wanawapotosha watu kupitia baadhi ya matamshi yao.

Serikali ilisema kwamba vifaa vya kupigia kura, ikiwa ni pamoja na karatasi ambazo zimeanza kusafirishwa hii leo kwelekea kwenye vituo vya kupigia kura katika maeneo mbali mbali ya nchi, vitapewa ulinzi mkali.

Shehena ya mwisho ya karatasi za kupigia kura iliwasili Junamme usiku katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta kutoka dubai ambako zilikuwa zikichapishiwa.

Imeandikwa na BMJ Muriithi akiwa Nairobi, Kenya.