Kenya, Uingereza kushirikiana kutokomeza ufisadi

Rais Uhuru Kenyatta na Waziri Mkuu Theresa May

Kufuatia mashauriano kati ya Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May, aliyefanya ziara ya kikazi nchini Kenya Alhamisi, amesema nchi hizo mbili zimekubaliana kuimarisha juhudi za kupambana na ufisadi.

Uingereza imeahidi kurejesha mali inayo fungamana na ufisadi iliyofichwa nchini humo iwapo hilo litabainika.

Pia Kenya na Uingereza zitaendelea kupanua masoko yake ya bidhaa hata baada ya Uingereza kuondoka katika umoja wa Ulaya.

Mwandishi wa idhaa ya Kiswahili, VOA anaripoti kuwa miaka thelathini baadaye hatimaye, Waziri Mkuu wa Uingereza amefika Nairobi.

Theresa May anakuwa Waziri Mkuu wa pili wa Uingereza kutua Nairobi baada ya Margaret Thatcher kuzuru Nairobi mwaka wa 1988.

Ziara ya May ni kuboresha mahusiano ya nchi yake na Kenya wakati Kenya imepiga hatua muhimu katika uchumi wake.

Lakini pia anafika wakati Kenya inajaribu kupambana na ufisadi.

Kenya na Uingereza Alhamisi zimeweka mkataba wa kuhakikisha mali ya Kenya iliyofichwa katika mabenki ya Uingereza inarejesha Nairobi. Hili Rais Kenyatta akilisifia na kutaja kuwa kupambana na ufisadi ni kipaumbele katika serikali yake.

"Juhudi za kupambana na ufisadi ni kipaumbele katika awamu yangu ya mwisho madarakani pamoja na umoja wa nchi katika na kufanikishwa kwa agenda zetu nne za maendeleo," ameeleza Rais Kenyatta.

Kwa upande wake May ameahidi kushirikiana na Kenya kutokomeza mtandao wa mafisadi.

"Tumezungumzia athari ya ufisadi nchini Kenya.Naridhishwa na kujitolea kwenu kuondosha uozo huu katika nchi yenu, tunajiunga nanyi katika harakati hizi na leo tumeafikiana kuwa tutarejesha mali yoyote ya Kenya inayotokana na ufisadi iliyofichwa nchini mwetu ili iwafaidi wakenya," amesema Waziri Mkuu May.

Uingereza ndio nchi pekee ya kigeni inayowekeza zaidi nchini Kenya, na kutokana na hili Theresa May anasisitiza kuwa ziara yake nchini Kenya ni mpango mkakati wa Uingereza kuhakikisha kuwa ndio itakayokuwa nchi ya kipekee katika muungano wa kiuchumi wa G7 kuwekeza zaidi barani Afrika ifikapo mwaka wa 2022.

Aidha, Waziri Mkuu May amezisifia juhudi za majeshi ya Kenya kujitolea kuikomboa nchi ya Somalia

May amesema kuwa: "Uingereza inaendelea kutambua umahiri na kujitolea kwa wanajeshi wa Kenya walioko Somalia kupambana na Alshabaab.Nitatangaza ufadhili upya kuchangia juhudi za wanajeshi wa Amisom nchini Somalia, tunaongoza juhudi za mataifa ya ulimwengu kusaidia Amisom kupambana na ugaidi."

Rais Kenyatta ameeleza kuwa serikali ya Uingereza imeahidi kupanua soko lake la mauzo yasiyo tozwa ushuru kwa Kenya hata baada ya Uingereza kujiondoa kutoka Umoja wa Ulaya.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu Kennedy Wandera, Kenya.