Kenya, Uganda kusimamia mazungumzo kati ya Somalia na Ethiopia

Rais wa Uganda Yoweri Museveni (amesimama) na rais wa Kenya Dr. William Ruto katika ikulu ya rais ya Kenya. Mei 16 2024

Rais wa Kenya Dr. William Ruto, amesema kwamba ni jukumu la pamoja la viongozi wote wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhakikisha kwamba kanda nzima ina usalama na utulivu.

Akizungumza katika kikao cha 24 cha viongozi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, mjini Arusha, Tanzania, Ruto amesema haiwezekani kwa jumuiya kuvutia wawekezaji iwapo hakuna usalama na utulivu.

Ameongezea kwamba itakuwa vigumu kwa wakazi wa jumuiya kutembea nchi moja hadi nyingine na kufanya biashara iwapo hakuna amani, usalama na utulivu, akisema kwamba hiyo ndiyo sababu kubwa Kenya imewekeza zaidi katika kuhakikisha kwamba kuna usalama na utulivu Sudan Kusini, kwa kuzingatia ombi la rais wa Sudan Kusini Salva Kiir.

Ruto amezungumza muda mfupi baada ya kutawazwa kuwa mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kutoka kwa rais wa Sudan Kusini Salva Kiir.

Amefichua kwamba Kenya na Uganda zitaongoza juhudi za mazungumzo kati ya Ethiopia na Somalia ambazo zimekuwa katika mzozo wa diplomasia unaotishia utulivu katika eneo hilo.

Ethiopia, ambayo haina bahari na yenye maelfu ya wanajeshi nchini Somalia kupambana na kundi la kigaidi la Al-Qaeda, ina mgogoro wa kidiplomasia na serikali ya Mogadishu baada ya kufikia makubaliano na Somaliland kutumia sehemu ya bahari yake kwa shuguli za kibiashara na ulinzi.

Somalia imeitaja hatua hiyo ni kuingilia kati mipaka yake.